Mahakama Kuu ya Tanzania, imekubali kifungo cha miaka 30 jela walichohukumiwa Raia wa Poland, Damian Krzystof na mkewe mtanzania Eliwaza Pyuza Aprili 2021 baada ya kutiwa hatiani kwa kulima na kusafirisha bangi.
Nakala ya Hukumu ya rufaa hiyo imepatikana leo 2022,ambayo imetolewa na Jaji Safina Simfukwe wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi, ambaye alizitupa sababu 10 za rufaa za wafungwa hao waliokuwa wakitetewa na wakili Median Mwale.
Hukumu iliyowafunga wawili hao ilitolewa Aprili 9, 2021 na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Moshi, Bernazitha Maziku ambaye aliwatia hatiani kwa makosa hayo waliyoyafanya Februari 8,2020 na kuagiza pia mali zao zitaifishwe na serikali.
Mali hizo ni shamba lenye ukubwa wa hekari moja lililopo Njiapanda ya Himo wilaya ya Moshi walipokutwa wakijihusisha na kilimo cha bangi, pikipiki aina ya KTM Adventure yenye namba za usajili MC972 AAD na fedha taslimu shilingi milioni 26.7.
Hata hivyo, kupitia kwa wakili Mwale, wafungwa hao walikata rufaa wakisema Hakimu alikosea kisheria kuwatia hatiani wakilalamikia mambo kadhaa yakiwemo namna ya upekuzi na ukamataji mali nyumbani kwao ulifanyika usiku bila kuwapo amri ya mahakama.
Halikadhalika walidai hakimu alikosea kisheria kwa kupokea vielelezo mbalimbali licha ya mnyororo wa makabidhiano kuvunjika, washitakiwa kutopatiwa nakala ya maelezo ya mlalamikaji na Damian na kutoelewa vizuri lugha ya Kingereza na Kiswahili.
Hata hivyo hoja hizo zilipanguliwa na wakili mwandamizi wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Kassim Nassir aliyeiwakilisha Jamhuri, akisema sababu hizo hazina mashiko na kwamba ushahidi uliowatia hatiani washitakiwa ulikuwa ni mzito.
Katika hukumu yake, Jaji Simfukwe baada ya kupitia hukumu iliyotolewa na Hakimu Maziku na sababu za rufaa, mahakama imeridhika kuwa mnyororo wa vielelezo ulizingatia utaratibu wa kisheria na hauacha mashaka kwa upande wa mashitaka.
Kuhusu suala la lugha, Jaji alisema katika usikilizwaji wa shauri hilo kulikuwepo mkalimani na Damian alikuwa na wakili ambaye hakuwahi kuibua suala hilo wakati wa usikilizwaji lakini Damian alikuwa akiwasiliana na mkewe kwa lugha ya Kiingereza.
Akizungumzia suala la upekuzi, Jaji Semfukwe alisema mahakama ina maoni kuwa mazingira ya upekuzi na uchukuaji vielelezo yalikuwa na udharura na kwamba kama ungefanyika utaratibu wa kuomba kibali mahakamani, huenda taarifa zingevuja.
“Kwa kuhitimisha na baada ya kukuona kuwa sababu zote za rufaa zilizoletwa na warufani hazina mashiko, rufaa hiyo inakosa miguu ya kusimama hivyo inakataliwa. Kutiwa kwao hatiani na kifungo walichopewa kinabaki kama kilivyo,”alisema Jaji.
Raia huyo wa Poland na mkewe, walikamatwa Februari 8, 2020 nyumbani kwao eneo la Shirimatunda nje kidogo ya mji wa Moshi wakiwa na mashine za kuchakata bangi na pia walikutwa wakilima bangi hiyo katika kiwanja chao eneo la Njiapanda.
Mbali na maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) kukamata shamba hilo lenye ukubwa wa kati ya hekari moja na nusu likiwa na miche 729, pia walikuta bangi iliyochakatwa na kuchanganywa na asali na Jam.