Waziri wa Afya nchini Tanzania Ummy Mwalimu amesema pamoja na serikali ya nchi hiyo kuwekeza fedha nyingin katika kuboresha miundombinu, Vifaa tiba na dawa bado hali ya utoaji huduma katika hospitali na vituo vya afya vya seriakali ni mbovu.
Waziri huyo alitoa kauli hiyo jana jijini Dodoma nchini Tanzania wakati alipokuwa akifugua mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara ya Afya nchini humo.
“Wakati tunajisifia kuwa tumepata mafanikio, Watanzania wamekuwa wanatushangaa pamoja na kutumia fedha nyingi katika kuwekeza katika sekta hii, huduma bado ni mbovu.
“Hivi sasa serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya dawa lakini bado kuna malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kupata dawa katika hospitali na vituo vya afya vya serikali. Watu hawapati dawa, lakini suala la huduma kwa wateja bado ni kero kulinganisha na hospitali za binafsi,” alisema Ummy.
Waziri huyo ameshangazwa na kauli zinazotolewa ha watoa huduma za afya katika hospitali za Serikali kwa wagonjwa ukilinganisha na kauli za watoa huduma hizo kwa hospitali binafsi.
“Kwa nini daktari huyo huyo akiwa katika hospitali binafsi anakuwa na kauli nzuri kwa wateja, lakini akiwa katika hospitali za serikali anakuwa na kauli mbovu kwa wateja? Mgonjwa anakwenda hospitali binafsi anahudumiwa vizuri lakini huku kwetu huduma ni mbovu,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, aliwaagiza watumishi wa afya kuwa wabunifu katika kuweka utaratibu mzuri wa kutoa huduma kwa wateja ili kuongeza mapato.
“Watu wengi hivi sasa wanakwenda katika hospitali za binafsi kutokana na kupatiwa huduma nzuri. Lakini kama mtaweka mazingira mazuri, lazima wataanza huku badala ya kwenda katika sekta binafsi na ninyi kupata mapato ambayo yatawasaidia kuhudumia wale watu wa msamaha,” alisema.
Pia aliagiza kuandaliwa kwa utaratibu wa kila kituo cha afya au hospitali ya serikali kuwapo na duka la dawa ili kuondoa kero iliyoko hivi sasa ya wagonjwa kukosa dawa.
Akizungumzia kuhusu kufanya mapitio ya gharama za matibabu kwa hospitali na vituo vya afya vya serikali, alisema ndani ya miezi mitatu wanatarajia kutoa mwongozo utakaoelekeza kiasi cha malipo kwa huduma mbalimbali.
“Mwongozo uliopo ni wa muda mrefu na umepitwa na wakati. Sasa tunakwenda kufanya mapitio ya gharama kama mtu anataka kumwona daktari ni kiasi gani anapaswa kulipa kwa zahanati, kituo cha afya, hospitali za rufani za mikoa au zile za kanda ili kuondoa kero iliyopo hivi sasa ya watu kijipangia kiholela kiasi kikubwa cha fedha,” alibainisha.
Pia alisema katika uongozi wake kwenye wizara hiyo, vipaumbele vyake ni huduma bora za afya, bima ya afya kwa wote na huduma za kinga.
“Nataka katika awamu hii ambayo nimerudi Wizara ya Afya, tupimwe katika mambo haya. Ni lazima huu mchakato wa kila Mtanzania kuwa na bima ya afya, ukamilike kwa muda mfupi ili kuondoa changamoto za matibabu kwa fedha mkononi,” alisema.
Alisema lengo la wizara hiyo ni kutoa huduma bora za afya, kinga, vipimo, upasuaji, huduma za kansa na kukomesha malalamiko ya kukosa dawa kwa wagonjwa katika hospitali na vituo vya afya vya serikali.