Mkazi wa Kijiji cha Kising’a wilayani Kilolo, Frank Kigomba (31) amehukumiwa kwenda jela miaka 30 na kulipa fidia ya Shilingi 500,000 kwa kosa la kumbaka dada yake wa tumbo moja mwenye umri wa miaka 15.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi amesema tukio hilo la ubakaji lilitokea Januari 2, mwaka huu na kwamba tayari lilifikishwa mahakamani na hukumu imetolewa.
Bukumbi alisema mtuhumiwa huyo alienda chumbani kwa ndugu yake na kumuita, akimtaka amsaidie kuingiza mbao ndani ya pagale la nyumba anayojenga na kisha akamkamata kwa nguvu na kumvua nguo, kabla ya kumuingilia kwa nguvu na kumsababishia maumivu makali.
“Uchunguzi ulibaini kuwa mtuhumiwa huyo alishauriwa na mganga wa kienyeji kuwa akifanya mapenzi na ndugu yake atapata utajiri, alifikishwa mahakamani na kusomewa shitaka lake na kukiri kosa; na kuhukumiwa kifungo hicho,” alisema.
Katika tukio lingine alisema Isaya Lucas (25), amehukumiwa miaka 30 jela baada ya mahakama kuthibitisha kumbaka mwanafunzi wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 14 katika tukio la Aprili 4, 2022.
Alisema matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto hasa ubakaji na ulawiti mkoani Iringa yameendelea kuwa changamoto kwa sababu mbalimbali zikiwemo imani za kishirikina, magonjwa ya afya ya akili pamoja ulevi wa kupindukia na kuiomba jamii kutoa ushirikiano kuyadhibiti.