Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Hussein Bashe, amesema Serikali ya nchi hiyo ina mpango wa kuwainua wakulima na kukiinua kilimo cha Tanzania ili kufikia lengo la kukuza sekta ya Kilimo kwa 10% ambayo imepewa jina la 10/30.
Bashe amesema hayo katika mjadala wa pamoja uliowahusisha wadau wa Kilimo uliofanywa na Kituo cha televisheni cha Clouds jijini Dodoma Leo Katika ugawaji wa vitendea kazi kwa maafisa ugavi wa Kilimo wa Tanzania.
Amesema Ajenda ya 10/30 ni lengo ambalo wizara yake imejiwekea kulifikia mwaka 2030, ambapo kwa sasa Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano unaisha mwaka 2025 unaeleza kwamba sekta ya kilimo inatakiwa ikuwe kwa wastani wa 5.7% ikiwa ndio malengo yaliyowekwa kwa Miaka mitano.
“Kwa sasa hivi population yetu ni watu Mil 60. Tunatarajia kufika mwaka 2030 itaongezeka kukaribia watu Mil. 80. Unapokuwa na watu 28% wapo kwenye dimbwi la umaskini na uchumi wetu ulivyokaa 61% ya Watanzania wote wapo kwenye sekta ya kilimo ambayo inachangia 26% tu ya pato la Taifa maana yake waliopo mashambani ni 61% ya nguvu kazi ya Taifa,” amesema Bashe.
“Na wanaoshughulika na shughuli za mashambani na uzalishaji ni wastani wa 15%- 20%, Sisi kama wizara tumejiwekea malengo kwamba ifikapo 2030 sekta hii ikue kwa 10% tunaita agenda 10/30.” aliongeza.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Benki ya maendeleo ya Kilimo TADB-Frank Nyabundege, amesema Benki yake inahakikisha inawafikia wakulima wengi zaidi, kwa kutoa msaada kwenye miradi mikubwa ambayo italeta tija katika nchi ya Tanzania na kuhakikisha nchi inafaidika na Kilimo.
Amesema Benki ya maendeleo ya Kilimo ni benki ambayo kazi zake ni kutekeleza sera ambazo zinawekwa na nchi, na agenda ya 10/30 ni maagizo ambayo yanatakiwa kutekelezwa kwa kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kilimo cha kibiashara.
Leo maafisa ugani wa Kilimo wa Tanzania nzima wamepewa vitendea lengo likiwa ni kufikia lengo la Ajenda 10/30 ambapo mgeni rasmi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Vitendea kazi hivyo kwa Maafisa Ugani nchini humo ni pamoja na pikipiki 2,000, vifaa vya kupima afya ya udongo (soil agro scanner) 143, simu janja 384 na visanduku yva ufundi vya Maafisa Ugani 3,400.