Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limesema linamshikilia Derick Derick Junior(36) mkazi wa Salasala Kinondoni kwa tuhuma za kujeruhi na kutishia kwa silaa.
Taarifa ya Polisi imekuja siku moja baada ya tukio hilo kusambaa katika mitandao ya kijamii ikionesha picha ya mjongeo ambayo inamuonyesha mwanaume mmoja ambaye ametambulika kwa jina la Derick Derick Junior akimpiga mwanaume mwengine hadi kumjeruhi na kisha kumtishia silaa.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 27,2024 saa 12:30 maeneo ya Masaki “1245 night club” ambapo mtuhumiwa alimjeruhi mwanaume huyo aliyefahamika kwa jina la Julian Bujuru na kwa sasa anaendelea na matibabu.
“Polisi tunatoa taarifa kuhusiana na video zilizoonekana kwenye mitandao ya kijamii October 27,2024 zikionesha Mwanaume mmoja akitishia Watu kwa silaha ambapo tukio hilo baada ya uchunguzi ilibainika lilitokea October 27,2024 saa 12.30 asubuhi maeneo ya Masaki ‘1245 night club’ Kinondoni ambapo Mtuhumiwa alimjeruhi Julian Bujuru kwa kumpiga na kitako cha bastola pia kumjeruhi sehemu ya jicho na pua, Kitendo hicho hakikubaliki ni kinyume na sheria, aliyejeruhiwa anaendelea vizuri na matibabu”
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi ni kwamba kwa sasa inakamilisha taratibu za kisheria ili mtuhumiwa aweze kufikishwa mahakamani.
Aidha limetoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na pia halitasita kumchukulia hatua mtua yeyote anaemiliki silaa kutumia silaa hiyo kinyume na sheria na kwamba ina mamlaka ya kufuta leseni yake ya kuimiliki.
“Aidha Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka linakamilisha utaratibu wa kisheria ili Mtuhumiwa aweze kufikishwa katika Vyombo vingine vya Sheria haraka iwezekanavyo, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa Wananchi kuwa halitasita kumchukulia hatua Mtu yoyote anayemiliki silaha, atakayebainika kufanya matendo ambayo ni kinyume na sheria, kanuni na taratibu zilizoainishwa katika kibali chake cha kumiliki silaha”