, ,

Chadema yatangaza siku saba za maombolezo ya mauaji ya Oktoba 2025, yataka uchunguzi huru

Asia Gamba Avatar

hama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza siku saba za kumbukumbu na maombolezo ya watu waliouawa wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, huku kikitaka uchunguzi huru unaohusisha vyombo vya kimataifa na wadau huru wa kitaifa ili kuwezesha upatikanaji wa ukweli, haki na uwajibikaji.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Jumanne, Oktoba 27, 2026, muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, amesema maombolezo hayo yataanza Oktoba 29 hadi Novemba 4, 2026, ambapo bendera za chama hicho zitapepea nusu mlingoti kuashiria kuwakumbuka waathirika wa matukio hayo.

Oktoba 29, 2025, iliingia katika historia ya Tanzania kama siku iliyoshuhudia umwagaji mkubwa wa damu, baada ya zaidi ya watu 500 kuripotiwa kuuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa kufuatia ghasia zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu.

Matukio hayo yalitokea katika mazingira ya malalamiko ya muda mrefu kuhusu masuala ya kisiasa na utawala, yakiwemo madai ya Katiba mpya, pamoja na changamoto za kiuchumi na ugumu wa maisha. Mwaka mmoja baadaye, suala la uwajibikaji kwa vifo na majeraha yaliyotokana na matukio hayo bado ni miongoni mwa masuala yanayozua mjadala, huku kukiwa na wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru ili kubaini mazingira ya vifo hivyo, wahusika na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kisheria.

Mnyika amesema Kamati Kuu imeazimia kuendelea kudai uchunguzi huru kuhusu mauaji hayo na matukio yaliyofuatia, utakaohusisha vyombo vya kimataifa pamoja na wadau huru wa kitaifa, kwa lengo la kuhakikisha ukweli unajulikana, haki inatendeka na wahusika wanawajibishwa.

Aidha, amesema chama hicho kinataka majeruhi na familia zilizopoteza wapendwa wao kutokana na mauaji hayo kupewa fidia kama sehemu ya kutambua utu wao na kuonyesha kuwajali waathirika wa matukio hayo.

Katika maadhimio hayo, CHADEMA imepanga kufanya kumbukumbu maalum Novemba 3, 2026, kuanzia saa moja usiku, ambapo mishumaa itawashwa kwa idadi ya watu waliouawa, pamoja na shughuli nyingine za kuwakumbuka waathirika.

Mnyika amesema katika kipindi cha siku saba za maombolezo, chama hicho kitashirikiana na familia zitakazokuwa tayari, wanachama na wananchi kuwafikia familia za waathirika katika maeneo mbalimbali ili kuwapa faraja, upendo na mshikamano. Hatua hiyo pia itahusisha familia za watu walioachwa na ulemavu kutokana na matukio hayo.

Vilevile, amesema Kamati Kuu imepongeza na kuunga mkono hatua za taasisi za dini, zikiwemo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), za kuandaa misa na ibada maalum kwa ajili ya kuomboleza waathirika wa matukio hayo.

Amesema viongozi wa CHADEMA wa ngazi ya taifa, mabaraza ya chama, wajumbe wa Kamati Kuu na viongozi wa kanda wametakiwa kushiriki katika ibada na dua zilizoitishwa na taasisi hizo pamoja na zile zitakazoandaliwa na dini na madhehebu mengine Oktoba 29, 2026.

CHADEMA pia imewahimiza wanachama wake na wananchi kwa ujumla kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika matukio ya kumbukumbu na maombolezo yatakayoandaliwa na wadau mbalimbali, huku ikiwataka kuvaa mavazi meusi au vitambaa vyeusi na vyeupe kama ishara ya maombolezo.

Mbali na maadhimio hayo, Mnyika amesema Kamati Kuu imejadili masuala mengine yanayokihusu chama, yakiwemo mgomo wa kula unaoendelea kufanywa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu aliyeko gerezani, matukio ya utekaji yanayohusisha wanachama na wanaharakati, ikiwemo suala la Twaha Mwaipaya, pamoja na kukamatwa kwa viongozi wa chama hicho.

Hata hivyo, amesema maadhimio kuhusu masuala hayo mengine yataelezwa baadaye katika siku zijazo.

 

Our Correspondent Avatar