,

Gachagua awakemea viongozi wa ODM kwa kuharibu chama cha Raila

Victor Wanaswa Avatar

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amewashutumu baadhi ya viongozi wa chama cha ODM kwa kuhujumu urithi wa kisiasa wa aliyekuwa Waziri Mkuu Hayati Raila Odinga, akidai kuwa chama hicho kimepoteza umaarufu wake mwaka mmoja tu baada ya kifo chake.

Gachagua ambaye ni kiongozi wa chama cha DCP, amesema ODM imepoteza nguvu na ushawishi wake wa kisiasa, akilaumu baadhi ya viongozi ambao hakuwataja kwa majina kwa kile alichokitaja kama kusaliti misingi na maono ya Raila aliyoyajenga kwa miongo kadhaa.

Kwenye taarifa yake ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha Raila Odinga, Gachagua alisema inasikitisha kuona chama hicho kikififia kwa muda mfupi kiasi hicho akikitaja kuwa miongoni mwa urithi mkubwa zaidi wa kisiasa ulioachwa na aliyekuwa Waziri Mkuu.

Gachagua alisema baadhi ya wanasiasa waliomumiminia sifa kiongozi huyo baada ya kifo chake hawakuwa wakimheshimu alipokuwa hai, akiwakosoa kwa kile alichokitaja kama unafiki wa kisiasa wa hali juu.

Alitaja baadhi ya matamshi ya dharau na kejeli yaliyowahi kutumiwa kumwelezea Raila yakiwemo “kumwita mchawi” na “mtu wa kung’oa reli,” akisisitiza kuwa baadhi ya wanaomuenzi sasa ni miongoni mwa waliowahi kumdhalilisha.

Kiongozi huyo wa DCP alisema anaamini kuwa ni muhimu kutambua na kuthamini mchango wa viongozi wanapokuwa hai badala ya kusubiri hadi wafariki dunia ndiposa waanze kuwasifu.

Gachagua, hata hivyo alimsifu Raila kwa uwezo wake wa kujenga chama imara cha kisiasa na kuhamasisha wapigakura kuwachugua wabunge wenye tajriba na uwezo wa kuwatumikia wananchi.

Alisema anajitahidi kufuata nyayo za Raila katika kukijenga chama cha DCP kuwa vuguvugu imara la kisiasa litakalokuwa na nafasi muhimu katika mijadala ya kisiasa nchini kwa miaka mingi ijayo.

Aidha, aliwataka wanachama wa DCP na wakenya kwa ujumla kuwachagua viongozi wenye uwezo, akisisitiza kuwa taifa linahitaji wabunge wanaoweza kuwakilisha maslahi ya wapigkura wao kwa ufanisi.

Matamshi ya Gachagua yalijiri wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kifo cha Raila, ambapo alisema hakuweza kuhudhuria hafla hiyo licha yake kualikwa na mjane wa Raila, Ida Odinga.

Gachagu alisema alikuwa nchini Marekani kuhudhuria shughuli aliyokuwa amepanga awali, jambo lililomzuia kushiriki katika hafla hiyo ya kumuenzi na kumkumbuka aliyekuwa Waziri Mkuu.

Gachagu ni miongoni mwa viongozi wakuu wa kisiasa nchini ambao hawakuhudhuria hafla hiyo. Wengine ambao walikosa kufika ni pamoja na Rais William Ruto ambaye aalikuwa katika ziara ya maendeleo Bonde la Ufa, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi.

 

Our Correspondent Avatar