, , , ,

Kutoka uhaini hadi uchochezi, safari ya kesi ya Lissu

Asia Gamba Avatar

Kwa siku takribani 577, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipas Lissu, alikuwa mahabusu akikabiliwa na shtaka la uhaini, mojawapo ya makosa mazito zaidi katika sheria za Tanzania, ambalo adhabu yake inaweza kuwa kifo.

Kesi hiyo iliyofuatiliwa kwa karibu ndani na nje ya Tanzania, haikuwa tu shauri la jinai lililomhusu mwanasiasa mmoja wa upinzani. Iligeuka kuwa moja ya majaribio makubwa kwa mfumo wa sheria, haki za kisiasa, uhuru wa kujieleza na mazingira ya demokrasia nchini Tanzania.

Safari yake ilianza Aprili 9, 2025, alipokamatwa na polisi katika mji wa Mbinga, mkoani Ruvuma, siku sita baada ya kutoa hotuba iliyokuwa imejikita katika kampeni ya CHADEMA ya ‘No Reforms, No Election’ – hakuna uchaguzi bila mabadiliko.

Katika hotuba hiyo, iliyotolewa Aprili 3, 2025, katika makao makuu ya CHADEMA jijini Dar es Salaam, Lissu alizungumzia msimamo wa chama hicho wa kutaka mageuzi ya mfumo wa uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Kauli zake kuhusu kuzuia uchaguzi, kuhamasisha uasi na kuvuruga uchaguzi ndizo zilizokuja kuwa msingi wa mashtaka yaliyofunguliwa dhidi yake.

Hata hivyo, zaidi ya mwaka mmoja na nusu baadaye, Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ilipotoa hukumu Novemba 6, 2026, ilimwondolea Lissu shtaka la uhaini lakini ikamkuta na hatia ya kosa la uchochezi na kumhukumu kifungo cha miaka minne jela.

Uamuzi huo ulihitimisha kesi ya uhaini, lakini ukafungua ukurasa mwingine wa mapambano ya kisheria, baada ya CHADEMA kutangaza kuwa itakata rufaa na kuomba Lissu apewe dhamana akisubiri uamuzi wa rufaa hiyo.

-Aprili 2025: Mwanzo wa safari ya kesip-

Mazingira ya kesi hiyo yanarudi Aprili 3, 2025, wakati Lissu alipokuwa akizungumza katika mkutano wa chama chake uliofanyika makao makuu ya CHADEMA jijini Dar es Salaam.

Wakati huo, chama hicho kilikuwa kikiendesha kampeni ya kudai mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, kikisisitiza kuwa uchaguzi haupaswi kufanyika bila kurekebishwa kwa kasoro zilizokuwapo katika mfumo wa uchaguzi nchini.

Katika hotuba yake, Lissu alitumia kauli zilizokuwa zikihusisha kuzuia uchaguzi, kuhamasisha uasi na kuvuruga uchaguzi kama njia ya kushinikiza mabadiliko.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa kauli hizo zilikuwa na nia ya kuishinikiza Serikali na kuchochea wananchi kuzuia mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kwa upande wake, Lissu alikiri kutoa kauli hizo lakini akapinga tafsiri ya upande wa mashtaka, akisisitiza kuwa zilikuwa sehemu ya harakati za kisiasa za kudai mageuzi ya uchaguzi na si mpango wa kuipindua au kuitishia Serikali.

Siku sita baada ya hotuba hiyo, Aprili 9, 2025, polisi walimkamata Lissu mjini Mbinga, mkoani Ruvuma, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara.

Alisafirishwa kwenda Dar es Salaam na siku iliyofuata, Aprili 10, 2025, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako alisomewa shtaka la uhaini.

Kesi hiyo ilifunguliwa chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), kinachohusu vitendo vinavyolenga kutishia au kupindua Serikali kwa namna inayotajwa na sheria.

Kwa kuwa shtaka hilo halikuwa na dhamana, Lissu aliendelea kubaki mahabusu, awali katika Gereza la Keko na baadaye kuhamishiwa Gereza la Ukonga.

Hapo ndipo safari ya zaidi ya miezi 19 ya kuwa kizuizini ilipoanza rasmi.

-Kesi ya uhaini na mvutano kuhusu namna ya kuendesha mashauri-

Katika hatua za awali, kesi ilipokuwa Mahakama ya Kisutu, kulikuwa na mijadala mbalimbali kuhusu uchunguzi, mashahidi na namna ushahidi ungewasilishwa.

Julai 15, 2025, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga, aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa umekamilika.

Agosti 4, 2025, Mahakama Kuu iliruhusu mashahidi wa kiraia wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi kwa utaratibu wa kulindwa utambulisho wao. Hatua hiyo ilimaanisha kuwa baadhi ya mashahidi wangeweza kutoa ushahidi bila kuonekana moja kwa moja na umma.

Lissu alipinga utaratibu huo, akieleza wasiwasi wake kuhusu haki ya mshtakiwa kuzijua na kuzikabili hoja za mashahidi wanaomshutumu.Agosti 18, 2025, mahakama ilisimamisha matangazo ya moja kwa moja ya baadhi ya mwenendo wa kesi, ingawa vikao viliendelea kuwa vya wazi kwa umma.

Upande wa mashtaka uliwasilisha orodha ya mashahidi 30 na vielelezo tisa ambavyo ulitarajia kuvitumia kuthibitisha shtaka.

Septemba 8, 2025, kesi ilipofikia hatua ya awali katika Mahakama Kuu, Lissu aliibua pingamizi kuhusu mamlaka ya mahakama na kasoro alizodai kuwapo katika hati ya mashtaka.Pingamizi hizo zilikataliwa katika maamuzi yaliyofuata, na Septemba 22, 2025, kesi iliingia katika hatua ya kusikilizwa kwa utaratibu rasmi wa awali.

Katika kipindi hicho, Lissu aliendelea kusisitiza kuwa kauli zake zilikuwa sehemu ya haki yake ya kisiasa na kikatiba ya kutoa maoni kuhusu namna nchi inavyopaswa kuendesha uchaguzi.

Pia alitaka baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali na vyombo vya dola waitwe kutoa ushahidi katika utetezi wake.

-Oktoba 2025: Ushahidi waanza kutolewa-

Usikilizwaji wa ushahidi ulianza Oktoba 6, 2025, mbele ya jopo la majaji lililokuwa likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Miongoni mwa mashahidi wa kwanza alikuwa Naibu Kamishna wa Polisi George Bagyemu, aliyekuwa akihusishwa na uchunguzi wa kesi hiyo.

Hoja muhimu iliyojitokeza katika hatua hiyo ilihusu ushahidi wa kidijitali, hususan video iliyohusishwa na hotuba ya Lissu na uchapishaji wake kupitia Jambo TV.Upande wa mashtaka ulijaribu kuunganisha kauli za Lissu na ushahidi wa video, vifaa vya kielektroniki, kadi ya kumbukumbu na flash disk.

Hata hivyo, Oktoba 23, 2025, mahakama ilikataa baadhi ya ushahidi wa kitaalamu uliowasilishwa baada ya utetezi kuibua pingamizi kuhusu uwezo na utaalamu wa shahidi kuwasilisha ushahidi huo.

Shahidi Samwel Kaaya alikabiliwa na maswali kuhusu utaalamu wake katika eneo la uchunguzi wa video na vielelezo vya kidijitali.Lissu alijitetea pia kwa kuhoji uhalali wa namna ushahidi huo ulivyokusanywa, kuhifadhiwa na kuwasilishwa mahakamani.

Kesi ilisimama kwa muda kutokana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na mazingira yaliyofuata uchaguzi huo, kabla ya kuanza tena mwaka uliofuata.

Kesi ilipoanza tena Februari 9, 2026, mvutano mpya wa kisheria uliibuka baada ya upande wa mashtaka kutaka kuwasilisha ushahidi wa ziada kupitia Naibu Kamishna wa Polisi Amini Mahamba.

Lissu alipinga hatua hiyo, akidai kuwa ushahidi uliokuwa unapendekezwa haukuwasilishwa katika hatua zilizotakiwa kisheria na kwamba Serikali ilikuwa inajaribu kuongeza ushahidi nje ya utaratibu uliokubaliwa.

Februari 24, 2026, Mahakama Kuu ilikubali hoja za utetezi na kuondoa taarifa ya upande wa mashtaka iliyokuwa imewasilishwa chini ya Kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.Serikali haikukubaliana na uamuzi huo na kupeleka suala hilo Mahakama ya Rufani ya Tanzania.

Julai 3, 2026, jopo lililoongozwa na Jaji Augustine Mwarija, likisaidiwa na Majaji Zainabu Muruke na Amour Khamis, lilisikiliza hoja za pande zote.

Julai 30, 2026, Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali maombi ya Serikali, hivyo kuacha uamuzi wa Mahakama Kuu ukiwa umesimama.

Hili lilikuwa moja ya matukio muhimu katika safari ya kesi hiyo, kwa kuwa lilionesha namna mashauri ya kisheria kuhusu ushahidi yalivyochangia kuchelewesha mchakato wa kusikiliza kesi yenyewe.

Baada ya mapumziko marefu ya siku 167, kesi iliendelea tena Agosti 10, 2026.

-Serikali yafunga ushahidi, Lissu apelekwa kujitetea-

Agosti 17, 2026, upande wa mashtaka ulifunga ushahidi wake baada ya kuwaita mashahidi 17 kati ya 30 waliokuwa wameorodheshwa awali.

Miongoni mwa mashahidi waliotoa ushahidi ni maafisa wa polisi waliokuwa wakihusika na uchunguzi, akiwemo George Bagyemu na Amini Mahamba.

Lissu alitumia nafasi hiyo kuhoji uhusiano kati ya ushahidi uliowasilishwa na vipengele vya shtaka la uhaini.

Alisisitiza kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka haukuthibitisha kuwa alikuwa na nia ya kuitishia Serikali, kama ilivyodaiwa katika hati ya mashtaka.

Agosti 21, 2026, mahakama ilitoa uamuzi kuwa Lissu alikuwa na kesi ya kujibu.

Uamuzi huo ulimaanisha kuwa upande wa mashtaka ulikuwa umewasilisha ushahidi wa kutosha kumtaka Lissu ajibu tuhuma zilizokuwa zikimkabili. Hata hivyo, haukuwa uamuzi wa kuthibitisha hatia.

Lissu alichaguliwa kuwa shahidi wa kwanza wa utetezi wake mwenyewe na kuanza kutoa maelezo kuhusu mazingira ya hotuba yake, kampeni ya CHADEMA ya kudai mageuzi ya uchaguzi na tafsiri ya Serikali kuhusu kauli zake.

Ushahidi wake uliendelea kwa siku kadhaa hadi Agosti 28, 2026.Katika utetezi wake, Lissu alisisitiza kuwa alikuwa akipigania Katiba mpya, utawala wa sheria na mfumo wa uchaguzi ulio huru na wa haki.

Alipinga hoja kuwa alitoa kauli hizo kwa nia ya kuipindua Serikali, akieleza kuwa msimamo wake ulikuwa wa kisiasa na ulilenga kushinikiza mageuzi.

Katika hatua ya utetezi, Lissu aliwasilisha mashahidi mbalimbali, akiwemo Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika; Naibu Katibu Mkuu, Amani Golugwa; Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia; na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara, John Heche.

Mashahidi hao walitoa maelezo kuhusu mazingira ya kisiasa ya wakati huo, msimamo wa chama kuhusu mageuzi ya uchaguzi na namna kampeni ya No Reforms, No Election ilivyokuwa ikiendeshwa.

Lissu pia alitaka viongozi waandamizi wa Serikali na vyombo vya dola waitwe mahakamani kutoa ushahidi, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa Makamu wa Rais Philip Mpango, aliyekuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wa vyombo vya usalama.

Mahakama haikukubali baadhi ya maombi hayo, lakini iliruhusu kuitwa kwa baadhi ya viongozi wa vyombo vya dola, wakiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi Camillus Wambura, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Ramadhani Kingai na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jacob Mkunda.

Hata hivyo, viongozi hao hawakufika kutoa ushahidi.

Septemba 18, 2026, Lissu alifunga rasmi utetezi wake baada ya kueleza kuwa hakuwa na mashahidi wengine wa kuwaita.Alitoa maelezo kuhusu mawasiliano yake na baadhi ya viongozi hao na sababu zilizofanya ushahidi wao usipatikane.

-Je, Serikali ilithibitisha nia ya uhaini?-

Septemba 23 hadi 29, 2026, mahakama ilisikiliza hoja za mwisho za upande wa utetezi na Jamhuri.Kwa upande wa utetezi, hoja kuu ilikuwa kwamba Serikali haikuwa imethibitisha kipengele muhimu cha shtaka la uhaini, yaani nia ya Lissu kuitishia Serikali kwa namna inayotakiwa na sheria.

Lissu alisisitiza kuwa kukiri kutoa kauli hakumaanishi kukiri kuwa na nia ya kutenda kosa la jinai.Alieleza kuwa maneno yake yalipaswa kutafsiriwa katika mazingira ya mjadala wa kisiasa kuhusu uchaguzi na haki ya wananchi kudai mageuzi.

Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Nassoro Katuga, ulisisitiza kuwa ushahidi wa mashahidi 17 ulikuwa umethibitisha shtaka dhidi ya 

Lissu bila kuacha mashaka yanayoweza kumpa nafasi ya kuachiwa huru.

Jamhuri ilidai kuwa kauli za Lissu zilikuwa na lengo la kuhamasisha wananchi kuzuia uchaguzi na kwamba zilichochea vitendo vilivyoweza kuvuruga mchakato wa uchaguzi.

Kwa hiyo, pande hizo mbili ziliiachia mahakama jukumu la kuamua kama kauli hizo zilikuwa sehemu ya uhuru wa kujieleza kisiasa au zilivuka mipaka na kuwa kosa la jinai.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, mahakama ilitangaza kuwa hukumu ingetolewa Novemba 6, 2026.

-Novemba 6, 2026 siku iliyobadili mwelekeo wa kesi-

Ilikuwa Ijumaa, Novemba 6, 2026, siku ambayo kesi iliyokuwa imechukua siku 577 tangu Lissu akamatwe ilitarajiwa kufikia mwisho wake.

Usalama uliimarishwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, hususan karibu na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambako hukumu ilisomwa.

Lissu aliwasili mahakamani saa mbili na dakika 23 asubuhi, huku kukiwa na ufuatiliaji mkubwa kutoka kwa wanasiasa, wanaharakati, wanadiplomasia na waandishi wa habari.

Jopo la majaji watatu liliongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Katika uamuzi wake, mahakama ilimwondolea Lissu shtaka kuu la uhaini baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kipengele muhimu cha nia ya kuitishia Serikali.

Huo ulikuwa uamuzi mkubwa kwa kuwa shtaka la uhaini lilikuwa na adhabu ya kifo.

Hata hivyo, kuachiwa kwa shtaka hilo hakukuwa mwisho wa kesi kwa Lissu.

Mahakama ilitumia Kifungu cha 319 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kilichoiruhusu kumtia hatiani kwa kosa dogo linalohusiana na shtaka kuu pale ushahidi unapothibitisha kosa hilo.

Kwa msingi huo, mahakama ilimkuta na hatia ya uchochezi chini ya Kifungu cha 390 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Kwa mujibu wa mahakama, ushahidi uliowasilishwa ulionesha kuwa kauli zake za kuzuia na kuvuruga uchaguzi zilikuwa na athari ya kuchochea watu kushiriki katika vitendo vilivyolenga kuvuruga mchakato wa uchaguzi.

Jaji Ndunguru alieleza kuwa mahakama ilikuwa imeridhika kwamba kosa hilo limethibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.

Baada ya hatua hiyo, Lissu alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela.

Uamuzi huo ulizua maswali mapya ya kisheria: ikiwa mahakama imebaini kuwa ushahidi haukuthibitisha uhaini, ni kwa kiwango gani ilikuwa sahihi kutumia kifungu cha kosa dogo la uchochezi na kumtia hatiani bila shtaka hilo kuwa ndilo shtaka kuu lililokuwa likisikilizwa?

Hilo ndilo eneo ambalo sasa linatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mapambano ya rufaa.

-Lissu: Haya ni mateso ya kisiasa-

Baada ya kuondolewa kwa shtaka la Uhaini na kupewa kesi ya Uchochezi, Lissu alipinga uamuzi wa mahakama na kuuelezea kama sehemu ya mateso ya kisiasa.

Alisisitiza kuwa hakushtakiwa kwa kosa la uchochezi, bali kwa uhaini, na kuhoji namna mahakama ilivyofikia uamuzi wa kumtia hatiani kwa kosa ambalo, kwa mtazamo wake, halikuwa msingi wa kesi iliyokuwa ikisikilizwa.

Alieleza kuwa alikuwa amekaa gerezani kwa siku 577 akikabiliwa na tuhuma za uhaini, lakini mwisho wa kesi akakutwa na hatia ya kosa jingine.

Pia alieleza wasiwasi kuhusu afya yake na mazingira ya mahabusu, akitaja historia yake ya kufanyiwa upasuaji mara nyingi baada ya kushambuliwa kwa risasi mwaka 2017.

Katika hatua ya kutakiwa kutoa maelezo kabla ya hukumu ya adhabu, Lissu aliiomba mahakama izingatie historia yake ya kulitumikia taifa, hali yake ya kiafya na muda aliokuwa amekaa mahabusu.

Hata hivyo, mahakama iliamua kumhukumu miaka minne jela.

-Hukumu yazua mjadala nje ya Tanzania-

Uamuzi huo haukuishia ndani ya mahakama au katika siasa za Tanzania. Pia ulizua mjadala miongoni mwa viongozi na mashirika ya haki za binadamu katika ukanda wa Afrika Mashariki na kimataifa.

Shirika la Amnesty International lilikosoa hukumu hiyo, likisema mwenendo wa kesi ulikuwa na changamoto zinazohusu haki ya kusikilizwa kwa haki.Miongoni mwa mambo ambayo shirika hilo lilitaja ni madai ya Lissu kunyimwa mawasiliano ya faragha na mawakili wake, kusimamishwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya baadhi ya vikao na mazingira ya mahabusu.

Amnesty ilitaka mamlaka za Tanzania kutengua hukumu na kumuachia huru Lissu, ikisisitiza umuhimu wa kulinda uhuru wa kujieleza na haki ya kukusanyika kwa amani.

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, pia alihoji uamuzi wa kumtia hatiani Lissu kwa uchochezi baada ya kuachiwa kwa shtaka la uhaini.

Nchini Kenya, aliyekuwa Waziri wa Sheria na kiongozi wa People’s Liberation Party, Martha Karua, alitaka Lissu aachiwe huru, akihoji sababu za kuendelea kumweka gerezani baada ya kuondolewa shtaka kuu lililokuwa limemweka mahabusu kwa muda mrefu.

Aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga, naye alikosoa mwenendo wa kesi na kutaka Lissu aachiwe huru.

Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, pia alieleza wasiwasi wake kuhusu mashtaka yaliyokuwa yanamkabili Lissu, akisema harakati za kudai mageuzi ya mfumo wa uchaguzi hazipaswi kutafsiriwa moja kwa moja kama uhalifu.

Kwa upande mwingine, Umoja wa Kimataifa wa Vyama vya Kidemokrasia (International Democracy Union – IDU), ambao Lissu ni Makamu Mwenyekiti Mtendaji, ulilaani hukumu hiyo na kuitaka Tanzania kutengua hatia na kumuachia huru.

Hata hivyo, maoni ya mashirika na wanasiasa hao ni tathmini zao kuhusu hukumu na mwenendo wa kesi, si maamuzi ya mahakama yanayobadilisha hukumu iliyotolewa.

-Kesi ya Lissu na mustakabali wa demokrasia Tanzania

Zaidi ya hatma ya Lissu binafsi, kesi hiyo imeibua maswali mapana kuhusu nafasi ya upinzani katika mfumo wa kisiasa wa Tanzania, uhuru wa kujieleza na namna sheria za usalama zinavyoweza kutumika katika mazingira ya ushindani wa kisiasa.

Lissu alikamatwa wakati wa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambao ulifuatiwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Uchaguzi huo uliambatana na vurugu za Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata, ambapo Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan iliripoti kuwa watu 518 walipoteza maisha. Hata hivyo, mazingira ya vifo hivyo na uwajibikaji wa vyombo vya dola vimeendelea kuwa sehemu ya mjadala wa kitaifa na kimataifa.

Hukumu ya Lissu inafuatiliwa pia katika muktadha mpana wa hali ya kisiasa nchini, hasa kuhusu uwezo wa vyama vya upinzani kushiriki katika siasa, kukosoa Serikali na kudai mabadiliko ya kikatiba.

Kwa CHADEMA, changamoto iliyopo sasa si tu kupambana na hukumu ya mwenyekiti wake, bali pia kuendeleza shughuli za chama huku kiongozi wake akiwa gerezani.

Kwa Serikali, kesi hiyo imeacha mjadala kuhusu namna ya kusawazisha utekelezaji wa sheria, usalama wa taifa na haki za kisiasa za wananchi.

Kwa Mahakama ya Rufani, hatua inayotarajiwa itakuwa fursa ya kuchunguza hoja za kisheria zitakazowasilishwa na upande wa utetezi na kuamua kama hukumu ya Mahakama Kuu ilikuwa sahihi kwa mujibu wa sheria.

-Safari haijaisha-

Novemba 6, 2026, ilifunga ukurasa wa kesi ya uhaini dhidi ya Tundu Lissu, lakini haikufunga mapambano yake ya kisheria.

Baada ya kukaa mahabusu kwa siku 577 akikabiliwa na uwezekano wa adhabu ya kifo, sasa anakabiliwa na kifungo cha miaka minne baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la uchochezi.

CHADEMA imetangaza kupinga uamuzi huo kwa njia ya rufaa na kutaka Lissu apewe dhamana wakati mchakato huo ukiendelea.

Hivyo, macho ya wafuasi wa CHADEMA, wadau wa haki za binadamu, wanasiasa wa Afrika Mashariki na jumuiya ya kimataifa sasa yanaelekezwa katika hatua inayofuata ya kesi hiyo.

Swali kubwa linalobaki ni kama Mahakama ya Rufani itakubaliana na tafsiri ya Mahakama Kuu kuhusu kosa la uchochezi, au itakubali hoja za utetezi na kubadili uamuzi huo.

Kwa sasa, jambo moja liko wazi: hukumu ya Novemba 6 haikuwa mwisho wa safari ya Tundu Lissu katika mahakama za Tanzania. Ilikuwa mwanzo wa sura nyingine ya mapambano ya kisheria ambayo matokeo yake yanaweza kuwa na athari zaidi ya hatima ya mwanasiasa mmoja, na kugusa mjadala mpana kuhusu haki, demokrasia na utawala wa sheria nchini Tanzania.

 

Our Correspondent Avatar