, , ,

Upinzani Kenya watoa masharti mapya kwa IEBC kabla ya Uchaguzi wa mwaka wa 2027

Victor Kayanda Avatar

Muungano wa upinzani nchini Kenya umetangaza kuwa umeandaa Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi wa mwaka wa 2026, unaolenga kurejesha kifungu cha 39 cha Sheria ya Uchaguzi na kuweka mfumo wa kisheria utakaohakikisha uchaguzi wa huru na haki.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyomo kwenye Mswada huo ni kuondolewa kwa kituo cha kitaifa cha kujumuisha matokeo ya Urais katika ujumbi wa Bomas Jijini Nairobi. Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, amesema kituo hicho hakipo katika katiba ya Kenya na kukitaja kama eneo la uhalifu.

“Mahakama iliamua kuwa matokeo yanayotangazwa katika vituo vya kupigia kura ndiyo matokeo ya mwisho, na jukumu pekee linalosalia ni kuyajumuisha.” Alisema Maraga.

Suala lingine la kimsingi ambalo wameibua ni kusafishwa kwa sajili ya wapiga kura. Wamesema Sheria inaitaka IEBC kufanya ukaguzi na kusafisha sajili ya wapigakura kila baada ua uchaguzi mkuu. Hata wameshikilia kuwa tume hiyo haifanya hivyo na badala yake imekuwa ikiandaa mikutano ambayo haina manufaa katika mchakato mzima wa maandalizi ya uchaguzi.

Hata hivyo suala tata ambalo pia wameibua ni kuhusu upeperushaji wa matokeo ya uchaguzi wa Urais moja kwa moja kutoka kwa vituo vya kupigia kura hadi katika vituo vya kujumlishia matokeo, wakisema hatua hiyo itaimarisha uwazi na kuzuia uwezekano wa kuhitilafiana na matokeo. Wamepinga vikali kauli iliyotolewa na mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon kwamba hatua hiyo itagharimu tume hiyo fedha zaidi wakisema wataalamu wa kiteknolojia wamesema hilo si kweli.

“Tuna ushauri kutoka kwa wataalamu unaopinga madai hayo, wakisema kuwa jambo hilo linawezekana kutekelezwa. Kwa hakika, iwapo IEBC itaruhusu vyombo vya habari kufika katika vituo ambako matokeo yanabandikwa, vyombo hivyo vinaweza kuwasilisha matokeo hayo moja kwa moja kwa umma.” Aliseme Maraga.

Mapendekezo mengine yaliyo katika Mswada huo ni pamoja na ununuzi wa mitambo ya uchaguzi kufanywa kwa uwazi, uajiri wa maafisa wa uchaguzi kwa njia ya uwazi na ulinzi wa mawakala wa vyama vya kisiasa katika vituo vya kupigia kura.

Wakizungumza na wanahabari jijini Nairobi, wametishia kuhamasisha wakenya kushiriki maandamano ya kitaifa kuanzia mwezi Januari mwakani iwapo IEBC itadindaa kushughulikia mapendekezo hayo.

Aidha viongozi hao walisusia mkutano na Tume hiyo uliokuwa umepangwa kufanyika Jumatano alasiri, wakimtuhumu Rais William Ruto kwa kuingilia uhuru wa tume hiyo na kushindwa kushughulikia masuala waliyoibua kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alidai kuwa mkutano huo ulikuwa umeandaliwa na Wizara ya Usalama wa Ndani, akihoji sababu ya maafisa wa serikali kuzungumza kwa niaba ya tume huru ya uchaguzi.

 

 

Our Correspondent Avatar