,

Idadi ya waliofariki nchini Kenya kwenye ajali ya barabara Mtito Andei yafikia 22

Victor Wanaswa Avatar

Idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali iliyotokea katika barabara kuu ya Nairobi kuelekea Mombasa nchini Kenya imefikia watu 22. Hii ni baada ya watu wenginbe wawili kuaga dunia wakipokea matibabu.

Ajali hiyo ya Jumapili mwendo wa saa moja asubuhi, ilitokea eneo la Kanga karibu na Mtito Andei baada ya basi la abiria kugongana ana kwa ana lori.

Kamishna wa kaunti ya Makueni Abdullahi Khalif awali alikuwa amethibitisha kuwa watu 20 waliaga dunia kabla ya idadi hiyo kupanda,

Kamishna huyo alisema kuwa idadi ya waliofariki inaweza kuongezeka. Aidha, inaripotiwa kuwa basi hilo lilikuwa linasafirisha abiria kutoka kwenye hafla ya mazishi wakati wa ajali hiyo ilipotokea.

Maafisa wa polisi walisema watu wengine kadhaa walipata majeraha na kukimbizwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Mtito Andei kwa huduma za matibabu huku miili ya waliofariki ikihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo.

Mazingira yaliyozunguka ajali hiyo bado hayajafahamika wazi. Ingawa mwendo kasi uliwahi kutajwa hapo awali kama sababu kuu inayochangia ajali za barabarani nchini Kenya.

Ajali hiyo imetokea wiki tatu baada ya watu 17 kufariki katika ajali nyingine kwenye barabara hiyo hiyo, inayounganisha mji mkuu, Nairobi, na mji wa Pwani wa Mombasa.

Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama nchini Kenya (NTSA) ilisema kuwa sehemu ya barabara hiyo ambapo ajali ilitokea imetambuliwa kama “eneo hatari kwa ajali” na kwamba mapendekezo yalikuwa yametolewa kushughulikia masuala ya usalama.

Our Correspondent Avatar