, , ,

Obama amkashifu Trump kwa sera zake akiwapigia debe wagombea wa chama chake

Victor Wanaswa Avatar

Aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama, amemkosoa vikali Rais Donald Trump, akilaumu utawala wake kwa kuongezeka kwa gharama ya maisha na kuanzisha vita vya Iran, huku akiendesha kampeni za kuwaunga mkono wagombea wa chama cha Democratic kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula ulioratibiwa kufanyika Novemba 3.

Rais wa sasa alichagua kufanya maamuzi mabaya mno,” Obama alisema akiwa Cleveland, Ohio ambapo alimpigia debe aliyekuwa seneta wa chama cha Democrate.

Obama alitoa matamshi hayo wakati wa mikutano ya kisiasa maeneo ya Ohio na Michigan, akiwahimiza wapiga kura kuwaunga mkono wagombea wa chama chake katika juhudi za kurejesha udhibiti wa Bunge la Marekani, ambalo kwa sasa linaongozwa na chama cha Republican chake Trump.

Akiwahutubia wafuasi wake mjini Cleveland, Ohio, Obama alimlaumu Trump kwa kufanya maamuzi mabaya, hasa kuanzisha vita dhidi ya Iran, ambavyo amesema vimechangia kupanda kwa gharama ya maisha.

Vita hivyo vimesababisha kupanda kwa bei ya mafuta duniani baada ya Iran kuzuia kwa kiasi kikubwa usafirishaji kupitia kivuko cha Hormuz kufuatia mashambulizi dhidi yake.

Obama alisema Wamarekani wanapaswa kutumia uchaguzi huo kuonyesha kutoridhishwa kwao na kile alichokitaja kuwa miaka miwili ya machafuko, ukatili, ufisadi na uzembe chini ya utawala wa rais Trump.

Katika mkutano huo, Obama alikuwa akimfanyia kampeni seneta wa zamani wa chama cha Democratic, Sherrod Brown, anayelenga kurejea katika Seneti kwa kushindana na seneta wa Republican Jon Husted.

Baadaye, Obama alielekea Michigan kumuunga mkono Abdul El-Sayed, mgombea wa chama cha Democratic anayekabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mgombea wa Republican Mike Rogers katika kinyang’anyiro cha kuwania wadhifa wa Useneta.

Obama pia aliangazia umuhimu wa ushirikiano wa viongozi kutoka jamii mbalimbali, akisema Michigan inaweza kujivunia kuwa na mwanasiasa Mwislamu na seneta Myahudi wanaowatetea wananchi katika Seneti ya Marekani. Alikuwa akimrejelea El-Sayed pamoja na seneta wa Democratic Elissa Slotkin, ambaye hatashiriki uchaguzi huo mwaka huu.

Hata hivyo, Trump alimjibu Obama kupitia mtandao wake wa kijamii akimtaja kuwa rais asiye na uwezo na kumshutumu kwa kuipa Iran mabilioni ya dola kupitia makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.

Obama alikuwa aliyeshindwa na kazi! Aliliba Iran Mabilioni ya Dola za Marekani na kuwapa mbinu ya kujipatia silaha za kinyuklia,” Trump alisema.

Makubaliano hayo, yaliyofikiwa wakati wa utawala wa Obama, yaliipa Iran unafuu wa vikwazo vya kiuchumi kwa masharti ya kupunguza kwa kiasi kikubwa shughuli zake za nyuklia. Trump alijiondoa katika makubaliano hayo wakati wa muhula wake wa kwanza na kurejesha vikwazo vikali dhidi ya Iran.

Obama pia aliwahimiza wapiga kura kutumia fursa ya upigaji kura wa mapema ambao tayari umeanza katika majimbo hayo mawili, akiwataka kutochelewesha uamuzi wao.

Katika Ohio, chama cha Democratic kinatarajia kufanya vizuri katika kinyang’anyiro cha ugavana, ambapo Amy Acton anakabiliana na Vivek Ramaswamy wa Republican, aliyewahi kuwania urais mwaka 2024.

Obama pia alikosoa miradi ya ukarabati na mapambo katika Ikulu ya White House chini ya Trump, akitania kuwa mwonekano wake sasa unafanana na jengo lililopambwa kupita kiasi.

Wakati huohuo, kura za maoni nchini Marekani zinaashiria kuwa chama cha Democratic kinaweza kurejesha udhibiti wa Baraza la Wawakilishi, ingawa kinakabiliwa na ushindani mkubwa zaidi katika kinyang’anyiro cha Seneti.

Uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani unatarajiwa kufanyika Novemba 3, huku vyama vikuu viwili vikishindania udhibiti wa vyombo vya kutunga sheria na mwelekeo wa kisiasa wa taifa hilo.

 

 

Our Correspondent Avatar