Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma amekitaka Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kuwasimamia wanachama wake ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili na uaminifu katika muktadha mzima wa utoaji haki nchini.
Prof. Juma ametoa wito huo leo tarehe 3 Julai, 2024 baada ya kuwakubali na kuwapokea Mawakili wa Kujitegemea 555 kwenye hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Maadili ndiyo yatadumisha taaluma ya uwakili, uanasheria. Mkiweza kusimamia maadili nyinyi wenyewe hakuna mtu yoyote ambaye atawaingilia. Utatudumu kwenye taaluma ya Uwakili kama utakuwa mwadilifu,” amesema.
Jaji Mkuu amebainisha kuwa Mahakama ya Tanzania haitakuwa tayari kufumbia macho vitendo vya utovu wa nidhamu vya Mawakili.
Ameziagiza Kanda (Chapter) za TLS na Kamati ya Kitaifa ya Maadili ya Chama hicho kufanya kazi yake kikamilifu.
“Nawaomba Majaji tuanze kutumia mamlaka yetu kwa niaba ya wananchi, chini ya Sheria ya Mawakili, kama Kamati na Chapter hizi hazitafanya kazi zake. Tusipofanya hivyo siyo tu heshima ya TLS itashuka, bali pia heshima ya Mahakama nayo itashuka,” amesema.
Amewakumbusha Mawakili hao kuwa kila taaluma au chama, mfano Chama cha Mawakili Tanganyika wana kanuni zinazosimamia maadili, hivyo akahimiza kanuni hizo ziwaongoze katika shughuli zao za kila siku.
Prof. Juma alieleza pia kuwa kama taratibu za taaluma yao zilivyo, kila Wakili anatakiwa kujiunga katika Chapter, ambazo ndiyo husimamia maadili yao na kuwasilisha taarifa kwenye Kamati ya Kitaifa ya Maadili kama kuna Wakili anaenda kinyume na maadili ya kazi yake.
Ameonya kuwa Mahakama kama mwakilishi wa wananchi itahakikisha maadili yanasimamiwa ipasavyo kama jukumu hilo halitatekelezwa kikamilifu na Chapters na Kamati ya Kitaifa ya TLS.
Jaji Mkuu amebainisha pia kuwa Ofisi yake, Jaji Kiongozi na Majaji Wafawidhi wamekuwa wakipokea malalamiko dhidi ya vitendo vya utovu wa maadili kuhusu Mawakili.
Alitoa mifano michache, ikiwemo Wakili kukataa kurudisha kwa mteja wake nyaraka halisi za shauri. Mhe. Prof. Juma amesema kuwa nyaraka zote za shauri ni mali ya mteja, hivyo anapobadilisha Wakili au mkataba unapoisha zile nyaraka lazima zirudi kwake.
“Wananchi wamekuja kulalamika kwetu, wakisema kwamba hawana kumbukumbu ya mashauri yao kwa sababu Wakili amekataa kuwarudishia majalada na wangependa kupata Wakili mwingine. Huo ni utovu wa nidhamu na itakuwa vizuri utovu wa aina hii ushughuklikiwe na Chama cha Mawakili wenyewe,” amesema.
Mfano mwingine ni Wakili kusimamia mkataba wa mauziano ya shamba na kupokea sehemu ya malipo na baadaye kupotea. “Hizi siyo hadithi za kutungwa, tunapokea hayo malalamiko. Mteja anakuja kuuliza unakuwa mkali,” Jaji Mkuu amebainisha.
Alieleza mfano mwingine ambao Wakili kushindwa kulipa kodi ya pango kwa mwenye nyumba. Mhe. Prof. Juma amesema hiyo ni aibu kubwa kwa Wakili kupanga na kufungua ofisi, halafu anakataa kulipa kodi ya pango kwa sababu yeye ni Wakili.
“Kuna lalamiko kwamba Wakili aliwasilisha hati ya maridhiano mahakamani akisema wadaawa wamekubaliana kulipana nje ya Mahakama, lakini wahusika hawajui. Wakili kutohudhuria mahakamani licha ya kulipwa, unachukua fedha huonekani, wakati mwingine kesi inafutwa. Hilo ni kosa la kimaadili,” amesema.
Hafla hiyo iliyoshereheshwa na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Tiganga Tengwa, imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama, akiwemo Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustafa Mohamed Siyani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mtendaji Mkuu, Msajili Mkuu na wajumbe wa menejimenti.
Alikuwepo pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, wawakili wa Mkurugenzi wa Mashtaka na Wakili Mkuu wa Serikali, wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria nchini, Majaji Wastaafu pamoja na ndugu na marafiki wa Mawakili hao wapya.