Kesi ya Polisi wanaodaiwa kufanya unyang’anyi wa kutumia silaha yapigwa kalenda, upepelezi ukiwa bado haujakamilika

Serikali imesema bado inaendelea na upelelezi katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayowakabili waliokuwa askari Polisi watatu.

Hayo yameelezwa leo Novemba 13, 2023 na Wakili wa Serikali, Pancrasia Protas katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu wakati kesi hiyo ya jinai namba 197/2023, ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa hao ni waliokuwa askari kanzu watatu mwenye namba  F 7149 D/Coplo Ramadhani Tarimo (42) maarufu kama Rasta na mkazi wa Kipawa; G 7513 D/Coplo Majid Abdallah(35) na mkazi wa Kunduchi na WP  6582 D/ Coplo Stella Mashaka ( 41) mkazi wa Railway.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya unyang’anyi wa kutumia silaha na kuiba shilingi milioni 90 , mali ya Grace Matage.

Wakili Protas alidai kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ajili ya kutajwa na kuangalia kama upelelezi umekamilika.

Katika hatua nyingine hii leo washtakiwa hao wameweza kupata mawakili wa kuwatetea ambapo mshtakiwa wa kwanza na wa pili wanatetewa na wakili Method Ezekiel,  huku mshtakiwa wa tatu akitetewa na wakili Peter Kibatala, ambaye kwa leo aliwakilishwa na wakili Grace Ndilla.

Wakili Ezekiel alidai mahakamani kuwa wateja wake bado hawajapewa hati ya mashtaka, hivyo aliomba upande wa mashtaka uwapatia wateja wake.

Hata hivyo, ombi hilo lilikubaliwa na upande wa mashtaka na kuahidi kuwapatia hati ya mashtaka washtakiwa hao.

Baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika, wakili wa utetezi Grace Ndilla anayemtetea mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo (Stella) ameieleza Mahakama kuwa wanakusudia kuwasilisha pingamizi la awali wakipinga hati ya mashtaka kuwa ina mapungufu.

Ndilla ambaye amemwakilisha Kibatala katika kesi hiyo alidai kuwa tarehe ijayo watawasilisha taarifa ya pingamizi hilo, hivyo wanaomba upande wa mashtaka kujiandaa kwa ajili pingamizi hiyo.

Wakili Ndilla baada ya kueleza hayo, hakimu Msumi alihoji kwa nini pingamizi hilo linakuja kwa njia ya mdomo na siyo kwa njia ya maandishi kama sheria inavyotaka.

Hata hivyo, hakimu Msumi alimuelekeza wakili Ndilla kuwasilisha taarifa ya pingamizi hilo kwa njia ya maandishi na siyo kwa njia ya mdomo ili upande wa mashtaka waweze kujibu hoja hizo.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Agosti 28, 2023 katika eneo la Kurasani, karibu na ofisi za Uhamiaji, lililopo Wilaya ya Ilala, ambapo siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja waliiba Sh90 milioni kutoka kwa Grace Donald Matage.

Inadaiwa kabla na baada ya kufanya wizi huo, walimtishia Grace kwa bunduki ili waweze kujipatia fedha hizo bila kikwazo.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Oktoba 31, 2023 wakikabiliwa na shtaka hilo

Hakimu Msumi baada ya kusikiliza kesi hiyo aliahirisha hadi Novemba 27, 2023 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa Sheria.