Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu, ameibua ameibua maswali kuhusu kutofautiana kwa ushahidi wa mpelelezi na maelezo aliyoyatoa katika hatua za awali za uchunguzi.

Katika mahojiano yake ya kuhojiwa na Lissu, shahidi huyo alikiri mara kadhaa kwamba baadhi ya mambo aliyoyataja mahakamani hayakuwepo katika maelezo yake aliyoyaandika polisi.
Lissu ambaye anashtakiwa kwa uhaini alimuuliza shahidi kuhusu jalada la uchunguzi wa tuhuma za uhaini linalomhusu, akitaka kujua iwapo jina lake lilikuwa limetajwa katika maelezo ya awali ya shahidi.
Shahidi alikiri kuwa jina la Tundu Lissu lilikuwepo katika maelezo hayo, lakini alikanusha kuwa aliandika kwamba aliona jalada lililomtaja Tundu Antipus Lissu alipofika kwa Naibu ZCO George Bagemu.
Utata mwingine uliibuka kuhusu uwepo wa mwanasheria katika timu ya uchunguzi. Shahidi alisema kulikuwa na mwanasheria, wakati shahidi mwingine, George Bagemu, ambaye alitangulia kutoa ushahidi, alisema hakukuwa na mwanasheria.
Lissu pia alimuuliza shahidi kuhusu video ya Jambo TV ambayo alisema aliitazama kwa karibu saa mbili. Hoja hiyo ilitofautiana na ushahidi wa Bagemu, ambaye alisema aliitazama video hiyo vipande vipande.
Shahidi alisisitiza kuwa yeye aliitazama video hiyo kwa karibu saa mbili.
Hata hivyo, Lissu alibainisha kuwa maelezo kadhaa ambayo shahidi aliyataja kuhusu video hiyo hayakuwepo katika taarifa yake ya awali, ikiwemo madai kwamba Lissu alikuwa amevaa vazi la kombati na kwamba nyuma yake kulikuwa na bendera ya Tanzania.
Shahidi pia alikiri kuwa maelezo kuhusu madai ya kuwepo kwa mipango ya kuvuruga uchaguzi, ikiwemo kutumia mawe na kufanya vurugu, hayakuandikwa katika maelezo yake.
Katika hatua nyingine, Lissu alimuuliza shahidi kama ushahidi wa video na taarifa ya uchunguzi wa kisayansi uliwasilishwa mahakamani. Shahidi alijibu kuwa hakuna kati ya vitu hivyo viwili alivyowasilisha.
Maswali hayo yaliendelea kuibua hoja kuhusu msingi wa ushahidi unaotumika kuhusisha hotuba ya Lissu na tuhuma za uhaini.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa mahakamani.