Maandamano ya kupinga serikali Madagascar yazuka upya, polisi watumia gesi ya machozi

Maelfu ya wananchi wamejitokeza tena Jumatatu (29.09.2025) katika maandamano makubwa ya kupinga serikali katika miji kadhaa ya Madagascar, yakiwemo maandamano makuu kwenye mji mkuu Antananarivo, ambako polisi walitumia gesi ya machozi kuwatawanya waandamanaji.

Wiki iliyopita maandamano ya siku mbili yaliibuka na kusababisha makabiliano kati ya vijana na polisi. Waandamanaji, waliyoitishwa kupitia mitandao ya kijamii na vuguvugu la “Gen Z”, walilalamikia kukatika kwa maji na umeme kunakolikithiri katika taifa hilo maskini.

Waandamanaji wengi walivalia nguo nyeusi na waliimba nyimbo wakimtaka Rais Andry Rajoelina ajiuzulu. Rajoelina, ambaye alichukua madaraka mara ya kwanza kufuatia mapinduzi ya umma mwaka 2009, aliondoka madarakani mwaka 2013, kabla ya kurejea tena kwa kushinda uchaguzi wa mwaka 2018 na kisha kuchaguliwa tena katika uchaguzi wenye utata wa mwaka 2023.

Vuguvugu hilo lilitoa tamko Jumapili usiku likitaka serikali pamoja na mkuu wa wilaya ya Antananarivo kujiuzulu. Kama ishara yao ya mapambano, vijana wa “Gen Z” wamechukua bendera ya maharamia kutoka kwenye katuni ya Kijapani One Piece  ishara ambayo pia imetumika katika maandamano ya vijana nchini Indonesia na Nepal.

Maandamano ya Alhamisi wiki iliyopita yalifuatiwa na uporaji usiku kucha kwenye maeneo mbalimbali ya mji mkuu bila uingiliaji wa polisi. Katika taarifa yake, “Gen Z” ilidai kwamba makundi ya watu waliolipwa kwa makusudi ndio waliohusika na uporaji huo ili kuchafua sura ya maandamano na kudhoofisha mapambano yao.

Maandamano pia yalienea mjini Antsiranana, kaskazini mwa Madagascar. 

Haya ndiyo maandamano makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 2023, wakati wananchi walipoandamana kabla ya uchaguzi wa rais uliosusiwa na vyama vya upinzani.

Katika hotuba ya video Ijumaa usiku, Rais Rajoelina alisema amemfuta kazi waziri wake wa nishati kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake, na akalitaja vurugu hilo kuwa “vitendo vya kuvuruga utulivu wa taifa”. Jumapili, akiwa mbele ya wakazi wa kitongoji cha wafanyakazi mjini Antananarivo, aliahidi “kurekebisha mambo na kuwa karibu zaidi na wananchi”.

Licha ya kuwa na rasilimali asilia, Madagascar inasalia kuwa miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani na pia moja ya nchi zilizo na viwango vya juu vya ufisadi. Kulingana na Shirika la Benki ya Dunia, mwaka 2022 karibu asilimia 75 ya wananchi waliishi chini ya mstari wa umasikini.