Majaliwa:Watanzania tulinde utamaduni wetu kwa faida ya vizazi vijavyo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wahakikishe wanalinda utamaduni na kujenga misingi ya kuhamasisha vijana na vizazi vijavyo kutambua na kuenzi historia na urithi wa Mtanzania.

Amesema kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kutunza utamaduni, mila na desturi kwa sababu utamaduni ni nguzo ya utambulisho wa jamii husika na ni muhimu kwa kizazi kijacho.

Amesema hayo (Jumapili, Oktoba 27, 2024) wakati akifungua Tamasha la Buhaya 2024 ‘Buhaya Festival’ lililofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

“Katika siku za sasa, ambapo teknolojia na utandawazi vinazidi kuimarika, ni rahisi kupoteza mila na desturi zetu, hivyo tunaposhiriki tamasha hili, tunajifunza na kuhamasisha jamii zetu kuhusu umuhimu wa urithi wetu wa kiutamaduni.”

Kadhalika, Majaliwa amewaasa wazazi, jamii na madhehebu ya dini kuendelea kuhimiza utunzaji wa maadili kwa kuzingatia mila na desturi ili kuepuka mmomonyoko wa maadili kwa vijana na jamii kwa ujumla. 

“Watanzania wote tuendelee kuheshimu na kuenzi tamaduni zilizo nzuri kama njia ya kuimarisha umoja, mshikamano na maendeleo ya kiuchumi,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri  Majaliwa ameagiza Mikoa yote nchini kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi iweke mipango ya kuandaa matamasha ya utamaduni kuanzia ngazi za Wilaya ili kuendeleza na kuhifadhi vivutio, mila na desturi za maeneo husika.