Makalla: Chanzo cha moto soko la Veterinary ni hitilafu ya umeme.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Amos Makalla, amesema chanzo cha moto uliosababisha kuteketea kwa Soko la Veterinary lililopo jijini humo eneo la TAZARA Wilaya ya Temeke, ni hitilafu ya umeme.

Makalla amesema hayo alipotembelea soko hilo leo kujionea uharibifu wa mali zilizoteketea moto, ambapo amesema taarifa za awali zinaonesha moto huo umeathiri takribani vibanda 453.

Amesema serikali inafanya taratibu za haraka, kuhakikisha kazi ya kurejesha miundombinu iliyoharibika inafanyika usiku na mchana, ili wafanyabiashara warudi kuendelea na biashara na kuahidi hakuna mfanyabiashara atakayeondolewa.

Ametoa pole kwa wafanyabiashara walioathiriwa na moto huo na kuwataka kuwa watulivu, wakati serikali yao inaendelea kutatua changamoto hiyo.

Kutokana na matukio ya moto kujirudia, Makalla ameendelea kutoa wito kwa viongozi wa masoko kuhakikisha, kila soko linakuwa na fundi umeme anayetambuliwa na TANESCO, halmashauri kuweka vifaa vya kudhibiti moto kwenye Kila soko.