Wakili na mwanaharakati kutoka kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), Flugence Masawe, ameonya kuwa matumizi ya mashtaka ya uhaini na ugaidi nchini Tanzania yanaweza kuathiri taswira ya nchi kimataifa, kuvunja imani ya wawekezaji na watalii pamoja na kuibua maswali kuhusu usalama wa mazingira ya kufanyika kwa matukio makubwa ya kimataifa.
Masawe amesema mashtaka hayo, ambayo ameyataja kuwa yana sura ya kisiasa, yanaweza kuleta madhara kwa uchumi wa nchi iwapo yataendelea kutumika katika mazingira ambayo yanatoa taswira kwamba Tanzania si sehemu salama kwa wageni na wawekezaji.
Akizungumza katika mkutano wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam, Alhamisi, Novemba 12, 2026, Masawe amesema wageni wanaopanga kutembelea Afrika huzingatia hali ya usalama katika kila nchi kabla ya kufanya maamuzi ya safari zao.
Ametoa mfano wa maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), akisema Tanzania inapojiandaa kuwa sehemu ya mwenyeji wa mashindano hayo huku kukiwa na matumizi ya mashtaka ya ugaidi, inaweza kuibua maswali kuhusu usalama wa nchi kwa washiriki na wageni wa kimataifa.
“Tunatumia makosa ya kisiasa lakini tunaharibu uchumi wa nchi. Kwa mfano tunaandaa AFCON huku tunasema tuna ugaidi. Je, ni sehemu salama kupeleka mashindano ya kimataifa?” amehoji Masawe.
Amesema badala ya kutumia mashtaka hayo kuwaumiza watu wanaokabiliwa nayo, Serikali inapaswa kuzingatia madhara yanayoweza kuikumba nchi kwa ujumla, ikiwamo kuathiriwa kwa sekta ya utalii na uwekezaji.
Masawe amedai kuwa baadhi ya mashtaka hayo hutumika kwa sababu ni makosa yasiyoruhusu dhamana, hali ambayo kwa maoni yake inaweza kumfanya mtuhumiwa kukaa gerezani kwa muda mrefu kabla ya kuthibitishwa kwa hatia yake.
“Yanatumika kwa sababu hayana dhamana ili ukae huko gerezani tu uumie. Ndiyo maana wanashindwa kuyathibitisha,” amesema.
Akizungumzia kesi ya uhaini iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Antipas Lissu, Masawe amesema mwenendo wa shauri hilo umeibua maswali kuhusu msingi wa ushahidi uliotumika kumfanya mahakama iamue kuwa alikuwa na kesi ya kujibu.
Amesema kwa kawaida, baada ya mahakama kuamua kuwa mshtakiwa ana kesi ya kujibu, ushahidi unaotolewa na upande wa utetezi hutathminiwa dhidi ya ushahidi wa awali wa upande wa mashtaka.
Kwa mtazamo wake, mwenendo wa utetezi wa Lissu ulionyesha kuwa kulikuwa na maswali kuhusu uzito wa ushahidi uliowasilishwa na Jamhuri.
Masawe pia amesema matumizi ya mashtaka ya uhaini yanaweza kutoa taswira kwamba Serikali haina utulivu au uimara wa kutosha, hasa pale watu wanapokabiliwa na tuhuma za kutaka kuipindua Serikali.
Amesema taswira hiyo inaweza kuwafanya watu wanaotathmini usalama wa nchi kusita kuitembelea au kuwekeza nchini.
Kuhusu kesi nyingine ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili Lissu katika Mahakama ya Kisutu, Masawe amesema hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu inaweza kuibua hoja za kisheria kuhusu uwezekano wa shauri hilo kuendelea.
Ametaja kanuni ya double jeopardy, inayohusu kutokumhukumu mtu mara mbili kwa kosa lilelile, akieleza kuwa kwa mtazamo wake, uamuzi wa Mahakama Kuu unapaswa kuzingatiwa katika kuamua hatima ya shauri la Kisutu.
Hata hivyo, amesema suala hilo linaachiwa mahakama husika kulitolea mwelekeo kwa kuzingatia sheria.
Akizungumzia kauli za taasisi na watu mbalimbali wanaotaka Lissu aachiwe huru baada ya hukumu, Masawe amesema matamko hayo hayawezi kubadilisha uamuzi ambao tayari umetolewa na mahakama.
Amesema njia ya kisheria iliyopo kwa Lissu ni kukata rufaa ili mahakama ya juu ichunguze hoja za kisheria zilizotolewa kuhusu mwenendo wa kesi, hukumu na adhabu aliyopewa.
Ameeleza kuwa pande zote mbili zina haki ya kukata rufaa, akisema hata Serikali inaweza kupinga sehemu ya uamuzi ambayo haijaridhishwa nayo, huku Lissu akiwa na haki ya kupinga kutiwa hatiani kwa kosa dogo na adhabu aliyopewa.
Masawe amewataka wananchi kuwa makini na maoni ya kisheria yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, akisema baadhi yanaweza kuathiriwa na misimamo ya kisiasa, chuki au mrengo wa mtu anayetoa maoni hayo.
Amesisitiza kuwa uchambuzi wa masuala ya sheria unapaswa kuzingatia misingi ya kisheria badala ya misimamo ya kisiasa.
Amesema pia watetezi wa haki za binadamu wanapaswa kubaki huru na kutetea haki bila kujali mtu anayehusika anatoka chama gani cha siasa.
Kwa mujibu wa Masawe, hoja zinazohusu utawala wa sheria zinapaswa kuzungumzwa kwa maslahi ya nchi, akitoa mfano wa matukio yaliyowahusu watu wenye misimamo tofauti ya kisiasa, akiwamo aliyekuwa kada wa CCM Humphrey Polepole na Alute Mughwai Lissu, kaka wa Tundu Lissu.
Amehitimisha kwa kusema kuwa mapendekezo ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande, yanapaswa kurejewa ili kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika mfumo wa haki jinai nchini.







