Mawaziri wa Jinsia na Masuala ya Wanawake katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) watakutana kesho nchini Malawi kwa ajili ya kufanya mapitio ya utekelezaji wa mipango ya jinsia na maendeleo ya jumuiya hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Sekretarieti ya Sadc kwa vyombo vya habari jana, mkutano huo utakaokuwa chini ya uenyekiti wa Waziri wa Jinsia, Maendeleo na Ustawi wa Jamii wa Malawi, Patricia Kaliati, utafuatilia utekelezaji wa Itifaki ya jumuiya hiyo kuhusu jinsia na maendeleo kwa kuzingatia nafasi ya wanawake katika siasa na utoaji uamuzi.
Taarifa hiyo ilisema kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa uwezeshaji kiuchumi wanawake (RMD-WEEP) 2020-2030 katika jumuiya hiyo, mawaziri hao watafanya mapitio ya mradi wa maendeleo ya viwanda na uwezeshaji wanawake kiuchumi.
“Mradi huo unaolenga kuongeza biashara zinazomilikiwa na wanawake na ushiriki wa wajasiriamali wa kike katika kuongeza thamani kwa sekta zilizochaguliwa na thamani ya minyororo kikanda,” ilisema.
Taarifa hiyo ilisema mawaziri hao pia watapitia utekelezaji wa mkakati na mfumo wa utekelezaji wa Sadc wa kushughulikia ukatili wa kijinsia (GBV) na kutathmini hali ya ukatili huo katika nchi za Sadc.