Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema aliyekuwa Mweneyekiti wa Chama Cha TLP, Augustine Mrema atakumbukwa kwa mengi katika nchi hii hasa katika harakati zake za kisiasa.
Mbowe ameyasema hayo leo Alhamis 25, 2022 wakati akizungumza nyumbani kwa marehemu Mrema katika shughuli ya mazishi ya mwanasiasa huyo katika Kijiji cha Kiraracha, Marangu, Mkoa wa Kilimanjaro.
Amesema Mrema alikuwa ni kiongozi ambaye alikuwa akikosoa na kupinga pale panapostahili na kusukuma vita ya kutafuta haki, demokrasia, uhuru na maendeleo ya Watanzania kupitia vyama vya siasa.
“Mrema alikuwa naibu waziri mkuu na waziri wa mambo ya ndani ya nchi katika nchi hii, pale alipoona kuna ulazima wa kukamilisha nafasi yake ili kuunga mkono juhudi za mageuzi katika Taifa alifanya hivyo,” amesema
“Alikuwa ni kiongozi ambaye alikuwa na nafasi kubwa ya kufanya maamuzi magumu katika harakati za kisiasa ni hakika tutammiss katika harakati za kisiasa hapa nchini,”amesema Mbowe
Mbowe amesema, “Mrema ni kilelezo bora cha watu wenye uthubutu, alionesha katika kipindi chote, aliweza kufanya uamuzi hata wengine walipoamini haiwezekani yeye alifanya.”
Amesema, walifanya naye kazi katika nafasi mbalimbali, “nahata alipotaka kufanya maamuzi tofauti na matajio ya wengi alifanya hivyo. Mrema ameacha jina kubwa katika nchi hii, amegusa kila kona ya nchi yetu na sisi viongozi wa mageuzi tuliotembea nchi hii tumeona nyayo zao.”
Mbowe amemaliza kwa kumshuruku Mungu kwa maisha ya Mrema.
Mrema alifikwa na mauti saa 12.15 asubuhi ya Jumapili Agosti 21, 2022 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu kuanzia Agosti 16, 2022.
Mbali na Mbowe baadhi ya viongozi waliohudhuria katika mazishi ya Mrema ni Waziri Mkuu mstaafu John Malecela, Mbunge wa zamani wa Moshi Vijijini, Thomas Ngawaiya.
Wengine ni, James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene anatarajiwa kumwakilisha Rais wa wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Mrema.