Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ameeleza kuwa mwezi huu umejawa na maombolezo kwa chama hicho kutokana na yanayoendelea kutokea dhidi ya wanachama wake ambapo hadi sasa baadhi yao hawajulikani walipo tangu walipotekwa na wasiojulikana huku wengine wakiishia mikononi mwa polisi kwa kesi zinazotajwa kuwa ni za uchochezi.
Mbowe ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza katika mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) uliofanyika Alhamisi, Septemba 19, 2024, katika Ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wenye lengo la kutathimini hali ya demokrasia nchini ikiwa ni sehemu ya tafakuri ya siku ya kimataifa ya siku ya demokrasia inayoaadhimisha kila inapofika Septemba 15 kila mwaka.
“Sisi katika chama chetu kwetu huu ni mwezi wa maombolezo, tunawashukuru Watanzania wote wa vyama vyote, wa taasisi mbalimbali, watu binafsi ambao wamelia na sisi, kwetu umekuwa mwezi mgumu mno”- amesema Mbowe
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa TCD amesema viongozi na wanachama wao wengine wamekuwa wakipotea katika mazingira ya kutatanisha hali inayozidi kuleta wasiwasi katika demokrasia nchini Tanzania.
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni kiongozi wa Chadema bwana Ali Kibao alichukuliwa na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi lakini siku moja baada ya tukio hilo mwili wake ulikutwa eneo la Ununio ukiwa na majeraha ikiwemo ya kumwagiwa tindikali usoni
Mbowe anasema katikati ya matukio hayo nchi inahubiriwa kujengewa amani na demokrasia jambo ambalo haliendani na matukio yanayotokea
Amesema ili demokrasia iwezo kuwepo nchini ni lazima iende sambamba na upatikanaji wa haki na uwepo wa utashi wa kisiasa hasa kutoka katika utawala wa nchi.
“Ili demokrasia iwe na maana lazima wakati wote itambue haki, ili kuweza kuwa na demokrasia na haki katika taifa lazima wakati wote paweze kuwa na utashi wa kisiasa na utashi huu wa kisiasa utoke zaidi kwa wale ambao wamepewa dhamana ya kuliongoza taifa letu”- amesema Mbowe na kuongeza
“Katika kipindi kifupi ambacho tulishaanza kuona matunda ya demokrasia katika taifa letu, kwamba kwa kiwango kikubwa uhuru wa kufanya siasa ikiwamo mikutano ya hadhara, maandamano yalifanyika nchi nzima kwa amani kubwa sana.Kwa ushirikiano mkubwa kati ya vyama vya siasa na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, kazi za siasa zikafanyika bila kuwa na tabu yoyote, tukaanza kuamini tunajenga utaratibu ulio bora, unaoliopeleka taifa letu katika chaguzi ambazo zitatupatia viongozi watokanao na mapenzi ya wananchi. Pamoja na hofu nyingi kutokana na kanuni na taratibu zetu zote za uchaguzi, angalau kwa nje palionekana pana utulivu na kazi za siasa zilifanyika”-
Aidha amesema kuwa pamoja na kwamba Katiba imeweka wazi suala la demokrasia na haki za binadamu lakini watawala wamekuwa wakivunja katiba na badala yake wamekuwa wakitumia nguvu ya mamlaka waliyonayo kuwaumiza wengine.
“Tunatamani Taifa hili liongozwe kwa Katiba iliyo bora ambayo itazaa sheria iliyo bora na vyote kwa pamoja vitatengeneza ustawi ulio bora kwa Raia wote, kwa muda mrefu katika Nchini yetu kumekuwa na utamaduni wa waliopo katika madaraka kuamini utashi wa Kiongozi Mkuu ndio unapaswa kuwa dira ya Taifa, haipaswi kuwa hivi”
Pamoja na hayo yote Mbowe amesisitiza kuwa haki itanedelea kupiganiwa hata ikiwa chini ya sheria mbovu zilizopo nchini.