Mbunge wa Viti Maalum(CCM), Subira Mgalu amependekeza wanaume wanaofanya vitendo vya ubakaji na ulawiti wahasiwe, ili kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Mbunge huyo ameyasema hayo kwa hisia kali ndani ya ukumbi wa bunge, wakati akichangia hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 mjini Dodoma leo.
Akichangia mjadala huo, Mgalu aliunga mkono serikali kuhusu mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto na kuongeza kuwa pamoja na mpango huu umepunguza matukio ya ukatil,i kuna haja kama taifa kujipanga kuangalia namna gani ya kushirikiana kupunguza matukio hayo.
Ameliambia Bunge kuwa takwimu za matukio hayo zinatisha, ukianzia Januari 2019 hadi sasa kumekuwa na matukio 19,000 ya ubakaji na katika hayo yaliyofikishwa mahakamani ni kama asilimia 75, huku ikionekana baadhi ya matukio hayafikishwi mahakamani.
Amesema kinachosikitisha zaidi matukio haya sasa yanafanyika mpaka ndani ya familia na kuongeza kuwa tatizo hili ni kubwa hasa matukio ya kulawiti watoto wa kiume, ambapo takriban matukio 3000 kati ya 3260 sawa na asilimia 94 yametokea kwa kipindi hicho.