Msaidizi binafsi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Antipas Lissu, David Jumbe, amesema alinusurika kuuawa baada ya kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana waliomshambulia, kumfunga pingu na kumpeleka kusikojulikana usiku wa kuamkia Alhamisi Mei 21, 2026 jijini Dar es Salaam.
Katika simulizi yake iliyojaa taharuki, Jumbe amesema tukio hilo lilianza majira ya saa nne usiku akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake Mabwepande, Bunju, akiwa ameambatana na rafiki yake aliyemtaja kwa jina la Macha.
“Gari aina ya Probox ilikuja kwa kasi ikatuzuia mbele, nyingine ikazuia nyuma. Wakashuka watu wengi, kama watano au sita. Wakafungua mlango wangu, wakamtoa yule niliyekuwa naye kwa nguvu, ndipo nikajua huu ni utekaji,” amesema Jumbe.
Kwa mujibu wa maelezo yake, watu hao walimvamia kwa nguvu huku baadhi yao wakijitambulisha kuwa ni askari polisi. Alisema alijaribu kupambana nao huku akipiga kelele kuomba msaada, lakini alizidiwa nguvu na kuingizwa kwenye gari.
“Walinizidi nguvu, wakaniweka nyuma ya gari na kunifunga pingu. Wakaendelea kunishambulia kwa mateke, ngumi na kitako cha bunduki. Walikuwa wakisema leo ndiyo siku yangu ya mwisho,” amesema.
Jumbe amesema damu zilizokuwa zikionekana mwilini mwake zilitokana na kipigo hicho, huku akidai alipigwa kichwani mara kadhaa wakati safari ikiendelea kuelekea maeneo ya Mbweni.
Katika hatua aliyodai ndiyo iliyookoa maisha yake, Jumbe amesema waendesha bodaboda waliokuwa eneo hilo walilifuatilia gari lililombeba jambo lililowatia hofu waliomshikilia.
“Walipoona bodaboda wanawafuatilia sana, mmoja alisema twende kituo cha polisi Mbweni. Lakini mwingine akasema, ‘Bosi amesema hii siyo kesi ya polisi, huyu anatakiwa amalizwe leo hii,’” amesema Jumbe ambaye mwili wake ulitawala majeraha huku mikono ikiwa imevimba kutokana na pingu aliyokuwa maefungwa na wanaodaiwa kuwa ni watekaji.
Amesema gari hilo baadaye liliingia eneo la msitu wa Mbweni karibu na eneo la usalama, ambapo waliomteka walishuka na kuanza kupiga risasi wakijaribu kuwatawanya bodaboda waliokuwa wakiwafuatilia.
“Walishuka wote upande mmoja wa gari wakiamini siwezi kutoka kwa sababu nilikuwa nimefungwa pingu. Nikajirusha kwa maumivu makali mpaka siti ya katikati, nikafanikiwa kufungua mlango upande mwingine na kukimbilia msituni,” amesema.

Kwa mujibu wa simulizi yake, alitembea kwa zaidi ya saa moja na nusu ndani ya msitu akiwa amejeruhiwa na bado amefungwa pingu mikononi, huku watu waliokuwa wakimshikilia wakidaiwa kuendelea kufyatua risasi wakimtafuta.
“Msitu ulikuwa mzito sana, nilikuwa napita kwenye miiba. Suruali ilinasa nikailazimika kuiacha kwa sababu sikuweza kujinasua nikiwa na pingu,” amesema.
Jumbe pia amedai kuwa mmoja wa watu waliomshambulia alikuwa amevaa sare za polisi huku wengine wakiwa wamevaa kiraia. Aidha, alidai mtu aliyekuwa akiongoza kundi hilo alikuwa akizungumza kwa lafudhi ya Kizanzibar.
-Chadema yazungumza-

Kauli hiyo imekuja wakati Chadema ikieleza kushtushwa na tukio hilo, likidai kuwa ni mwendelezo wa matukio ya vitisho na ufuatiliaji dhidi ya viongozi na wasaidizi wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Chadema, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Amani Golugwa, amesema tukio hilo linaashiria kushindwa kwa mamlaka za usalama kudhibiti vitendo vya utekaji.
“Tukio hili ni utekaji na ni uharamia. Limekuwa mahususi likimlenga David Jumbe ambaye ni msaidizi wa mwenyekiti wetu,” amesema Golugwa.
Kwa mujibu wa Golugwa, kwa muda mrefu kumekuwa na taarifa na fununu kuhusu Jumbe kufuatiliwa na watu wanaodaiwa kuwa askari polisi pamoja na wengine wasiokuwa na utambulisho rasmi.
Katika mkanganyiko ulioibua maswali zaidi, Golugwa amesema askari mmoja aliyefika makao makuu ya Chadema alfajiri ya Alhamisi alimweleza kuwa walikuwa wanamtafuta Jumbe ili wamfungulie pingu baada ya “kutoroka”.
“Swali langu likawa, ulijuaje amefungwa pingu? Na ametoroka akiwa mikononi mwa nani? Hayo maswali hayajajibiwa,” amesema Golugwa.
Ameongeza kuwa baadaye alizungumza kwa simu na askari mwingine ambaye ni ZCO Faustine Mafwele aliyemtaka Jumbe apelekwe kufunguliwa pingu, jambo ambalo amesema limeongeza mashaka kuhusu waliokuwa wakimshikilia.
-Polisi wazingira ofisi za Chadema-

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi lilizingira makao makuu ya Chadema yaliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam muda mfupi kabla ya chama hicho kuzungumza na wanahabari kuhusu tukio hilo.
Askari wenye silaha pamoja na magari ya polisi walionekana kuimarisha ulinzi katika eneo hilo huku baadhi ya waandishi wa habari na wanachama wakidai kuzuiwa kuingia ndani ya jengo hilo.
Tukio hili limeendelea kuleta gumzo mitandaoni na hasa kwenye majukwa ya wanaharakati wa haki za binadamu ambao wamekuwa na maswali yanayofanana huku hofu ya usalama wa raia ikiongezeka nchini.
Hata hivyo mpaka wakati taarifa hii inakwenda hewani Jeshi la Polisi halikuwa limetoa tamko rasmi kuhusu madai ya kutekwa kwa David Jumbe, mazingira ya tukio hilo wala tuhuma zozote zinazomkabili.