Mtoto Sofia Ndoni mwenye umri wa miaka mitatu amefariki dunia katika mazingira yanayodaiwa kuhusisha ukatili wa bibi yake mdogo, Christina Kishiwa, aliyekuwa akiishi naye katika Mtaa wa Nyakato, Kata ya Nyasubi, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wa taarifa, mtuhumiwa ambaye ni mama mdogo wa mama mzazi wa marehemu, anadaiwa kumpiga mtoto huyo maeneo mbalimbali ya mwili wake kisha kumkaba shingo na kusababisha kifo chake.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kulaani vikali vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Amesema jeshi la polisi linaendelea na msako wa kumtafuta mtuhumiwa huyo ili hatua za kisheria zichukuliwe.
“Vitendo hivi havikubaliki katika jamii. Tunatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa sahihi ili mtuhumiwa akamatwe haraka,” amesema Kamanda Magomi.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa chanzo cha tukio ni mtoto kutomuamkia bibi yake alipoinuka asubuhi, pamoja na kujikojolea, jambo lililodaiwa kuchochea hasira za mtuhumiwa na kupelekea kutumia nguvu zilizogharimu maisha ya mtoto.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Dk Michael Mushi, amesema walipokea mwili wa mtoto huyo usiku wa kuamkia jana Septemba 29, 2025, ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali.