Mwalimu wa Shule ya Msingi Mkombozi iliyopo halmashauri ya mji wa Njombe nchini Tanzania, Abel Bulugwe (21) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa darasa la sita anayesoma katika shule hiyo.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issah wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema mwalimu huyo alikwenda shuleni hapo kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo akitokea Chuo cha Ualimu Tandala kilichopo wilayani Makete mkoani Njombe.
Amesema alifundisha kwa miezi miwili kuanzia Januari mpaka Machi mwaka huu kisha kurudi chuoni kuendelea na masomo yake mpaka alipomaliza.
Amesema mwanzo mwa mwezi Juni mwaka huu alionekana mjini Njombe na ndipo alipokutana na mwanafunzi huyo akiwa amembeba mtoto akielekea saluni kwa ajili ya kunyoa nywele.
“Alimsindikiza mwanafunzi huyo mpaka saluni na matokeo yake mazungumzo yakawa mengi na kufikia hatua mwalimu huyo kuondoka na mwanafunzi mpaka sehemu alipofikia ambayo ni kwa rafiki yake,” amesema Issah.
Amesema mwanafunzi huyo alilala kwa mwalimu huyo pamoja na mtoto aliyekuwa naye na hakurudi nyumbani siku hiyo jambo lililosababisha watu wanaoishi naye jirani kuanza kumtafuta na hatimaye mwenyekiti wa mtaa alimuona na kutoa taarifa.
Amesema mwalimu huyo anashikiliwa na polisi akisubiri taratibu nyingine za kisheria zifuatwe ili aweze kufikishwa mahakamani kutokana na tuhuma zinazomkabili.