Search
Close this search box.
Africa

Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limezuia matokeo ya watahiniwa 540 kutoka vituo sita vya mitihani ndani ya jiji la Dar es Salaam baada ya kugundulika kufanya udanganyifu.

Wanafunzi hao wanatoka katika vituo vya Joylanda, Castle hill, Green Acress, Maktaba, Great Vision na Mtendeni.

Kwa mujibu wa taarifa ya baraza hilo, matokeo ya watahiniwa hao yanazuiwa hadi uchunguzi juu ya tuhuma hizo utakapokamilika.

“Wakibainika kufanya udanganyifu matokeo yao yatafutwa kwa mujibu wa kifungu Na. 4(8) cha Kanuni za Mitihani 2016 na endapo hawatabainika kufanya udanganyifu watapewa matokeo yao”.

Wakati huo pia baraza linazuia matokeo ya watahiniwa 179 ambao waliugua au walipata matatizo na kushindwa kufanya mitihani kwa masomo yote au baadhi ya masomo.

“Watahiniwa hudika watapewa fursa nyingine ya kurudia kufanya mtihani wa Kumaliza elimu ya msingi (PSLE) mwaka 2023 kwa mujibu wa kifungu 32(1) cha Kanuni za Mitihani,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine NECTA imezifungia shule 24 kuwa vituo vya mitihani ya Taifa baada ya kuthibitika kupanga kufanya udanganyifu katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.

Shule hizo ambazo ni sawa na asilimia 0.13 ya vituo vyote vya mitihani nchini, ndani yake zipo shule maarufu ikiwemo ya Musabe ya jijini Mwanza na St Anne Marie ya jijini Dar es Salaam na shule ya Rweikiza ya mkoani Kagera.

Hayo yameleezwa leo Desemba Mosi na Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amasi wakati akitangaza matokeo ya mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka 2022.

Akizitaja shule hizo ni Kadama shule ya msingi iliyopo Chato- Geita, Rweikiza (Bukoba), Kilimanjaro shule ya msingi (Arusha) Sahare (Tanga), Ukerewe (Mwanza), Peaceland (Mwanza), Karume (Kagera), Al-hikma (Dar es Salaam).

Nyingine ni Kazoba (Kagera), Mugini (Mwanza), Busara (Mwanza), Jamia (kagera), Winners (Mwanza), Musabe (Mwanza), Elisabene (Songwe), High Challenge (Arusha), Tumaini (Mwanza), Olele (Mwanza), Mustlead (Pwani).

Pia zipo shule za Moregas (Mara), Leaders (Mara), Kivulini (Mwanza) na St Severine (Kagera).

“Vituo hivi vimefungiwa kwa mujibu wa kifungu 4(8) cha kanuni za mitihani mwaka 2016 hadi hapo Baraza litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji wa mitihani ya kitaifa,” amesema.

Mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi ulihusisha watahiniwa zaidi ya 1.38 milioni nchi nzima.

Comments are closed