Search
Close this search box.
Africa

NCCR Mageuzi wagoma kushiriki kongamano la maridhiano lililoandaliwa na TCD

12

Chama  cha siasa cha upinzani nchini Tanzania cha NCCR-Mageuzi, kimesema hakitashiriki kongamano la haki, amani na maridhiano, lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kwa madai kuwa maandalizi yake hayajafuata utaratibu na baadhi ya mapendekezo yake kutofanyiwa kazi. 

Msimamo huo umetolewa leo na Mkuu wa Idara ya Sheria na Katiba wa chama hicho, Wakili Boniface Mwabukusi, ikiwa ni maazimio ya kikao cha kamati kuu iliyokutana jana Jumapili chini ya mwenyekiti wake, James Mbatia.

Itakumbukwa kuwa mbali na NCCR Mageuzi kutoa msimamo huo chama kikuu cha upinzani nchini humo chama cha CHADEMA  nacho kiliweka msimamo wake wa kutoshiriki mkutano huo kwa madai kuwa hakuna demokrasia ndani ya mkutano huo.

Kususiwa kwa kongamano hilo na vyama viwili vyenye nguvu kisiasa vitafanya vyama vitatu pekee vitakavyoshiriki ambavyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), ACT-Wazalendo pamoja na Chama Cha Wananchi (CUF).

Mwabukusi ametaja mapendekezo ya NCCR-Mageuzi, ambayo amedai hayajafanyiwa kazi kuelekea maandalizi ya kongamano hilo, ikiwemo la viongozi wa vyama vya siasa kuzungumza na Rais Samia kwa ajili ya kujadili ajenda zitakazojadiliwa katika kongamano hilo.

“Kwa bahati mbaya sana chama kilipokea barua ya kukijulisha utayari wa Rais kuonana na viongozi wa chama mnamo tarehe 18 Machi 2022, lakini kwa bahati mbaya ilipofika tarehe hiyo walipewa udhuru wa kuahirishwa wakaahidiwa kikao kitafanyika tarehe 21 Machi 2022, lakini tarehe 20 walipokea taarifa ya kuahirishwa tena,” amesema Mwabukusi.

Mwabukusi amesema “Tulishiriki kikao cha kamati ya ufundi ya TCD, tulihimiza umuhimu wa jambo hili, kwa bahati mbaya sana licha ya ahadi ya TCD kwamba viongozi watakutana na Rais kabla ya kikao cha Dodoma, haikutimizwa mpaka leo.”

NCCR-Mageuzi hakitashiriki kongamano hilo kwa kuwa ajenda zake zimeghushiwa, pamoja na vyama husika kutopewa taarifa za ajenda ambazo zinakwenda kujadiliwa.

“Msingi wetu ni kwamba, kikao cha Dodoma ni maziwa yaliyoghushiwa, hatuko tayari kuwapa Watanzania maziwa yaliyoghushiwa kwa kushiriki kikao. Haiwezekani kikao kimoja kina ajenda tofauti. Ukisoma taratibu za ratiba ya kingereza na kiswahili, ni mkutano wenye sura ya kinyonga ambayo ina lengo la kuwatega watakaohudhuria, kuridhia mambo ambayo wajumbe hawakupewa taarifa,” amesema Mwabukusi.

“Mpaka tunakwenda kwenye kongamano kila chama lazima kiwe kimepatiwa makabrasha ya ajenda, yapitiwe na kukubaliana kikamilifu ndiyo twende Dodoma. Kwa mara ya kwanza unaambiwa muswada ni wako hujui hata sentensi ya kwanza ina maana gani, huku ni kujigeyza kuwa madalali wa demokrasia,” amesema Mwabukusi.

Aidha, NCCR Mageuzi imemtuhumu Mkurugenzi Mtendaji wa TCD, Bernadetha Kafuko, amewaita wanachama wa NCCR-Mageuzi kushiriki kongamano hilo, kinyume cha sheria bila kuwashirikisha viongozi wao.

“TCD inajaribu kuchomoa watu kwenye vyama bila kufuata kanuni, chama ni taasisi unapotaka kufanya jambo unawafuata viongozi. TCD inachagua wanachama wa kawaida inawaambia wewe kiongozi wa NCCR njoo kikaoni. Tuna barua ya namna hiyo mtu anaambiwa wewe kiongozi uje. Chama hakina taarifa za kongamano ila mwanachama anazo,” amesema Mwambukusi.

Mwabukusi amesema, Kamati Kuu ya NCCR-Mageuzi, imeagiza wanachama wake walioko safarini kuelekea Dodoma kushiriki kongamano, warejee.

Mkutano wa TCD unatarajiwa kufanyika kesho na keshokutwa ambapo mgeni rasmi, anatarajiwa kuwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassani.

Mbali na mambo mengine Mwenyekiti wa TCD, ambaye pia ni Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo ndugu Zitto Kabwe, anatarajiwa kukabidhi kijiti cha uenyekiti wa TCD kwa Makamu Mwneyekiti wa Chama cha Mapinduzi ndugu Abdulrahman Kinana baada ya muda wake kuisha katika kuongoza TCD.

Comments are closed

Related Posts