Ndugai ataka chanjo ya Ukimwi itengenezwe

Aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai ameataka wataalam wa chanjo kwenda mbele zaidi katika kutazama uwezekano wa kutengeneza chanjo ya Ukimwi ili wananchi wafurahie maisha.

Ndugai ameibuka na hoja hiyo katika uzinduzi wa chanjo ya mifugo ya ugonjwa wa homa ya sotoka uliofanyika katika Wilaya ya Kongwa jijini Dodoma.

Hii ni mara ya kwanza kwa Ndugai kuonekana hadharani tangu alipojiuzulu nafasi ya Spika wa Bunge Januari 6 mwaka huu, huku wengi wakitaka kujua aliko baada ya kutoonekana bungeni.

Akizungumza mbele ya wafugaji katika uzinduzi huo uliofanywa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, Ndugai amesema kwa watu wa Kongwa ni furaha na neema ambayo wanapaswa kuishukuru Serikali ya awamu ya sita, juu ya kupatikana kwa chanjo hiyo ambayo inakwenda kuwa mkombozi kwa wafugaji wa Kongwa ambao walitaabika kwa muda mrefu..

Spika huyo wa zamani amesema kwa namna yoyote ufugaji wa mbuzi ulishashindikana katika wilaya hiyo lakini uwepo wa chanjo unakwenda kuwainua wafugaji akiwemo yeye kuwekeza zaidi kwenye mbuzi.

“Nampongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kutukumbuka watu wa Kongwa, Mheshimiwa Waziri tupelekee salamu na pongezi nyingi sana,”amesema Ndugai.

Katika hatua nyingine ameahidi kufanya kazi na kushauriana na Waziri Ndaki kwani amepangwa katika kamati ya Kilimo Mifugo na Maji ambayo ipo chini ya Wizara hiyo.