Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imelitaka Jeshi la Polisi nchini Tanzania kuhakikisha linaweka mbinu mbadala ili kutokomeza vitendo vya uhalifu mitaani vinavyofanywa na kundi la Panya Road.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Vita Kawawa ameyasema hayo leo Mei 5, 2022 wakati akiwasilisha maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Kawawa amesema vitendo vinavyofanywa na kundi hilo havifanyiki jijini Dar es Salaam peke yake bali vipo katika mikoa mbalimbali nchini, hivyo vinapaswa kukomeshwa.
Amesema askari wa Jeshi la Polisi wanapaswa wasimamiwe inavyostahili ili kuzingatia sheria, taratibu, miiko, weledi na maadili ya Jeshi la Polisi katika utendaji kazi wao.
“Dhana ya polisi jamii itekelezwe kwa ukamilifu katika kupambana na uhalifu hususani katika makazi ya watu, vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na kundi linalojiita panya road vinapaswa kukomeshwa kwa Jeshi la Polisi kuja na mbinu mbadala,” amesema.
Katika hatua nyingine Kawawa amesema Serikali inapaswa kusimamia maandalizi ya mpango mkakati wa muda mrefu na unaotekelezeka wa kuwarejesha katika nchi zao wafungwa waliomaliza vifungo na ambao bado wapo magerezani.
Amesema bila kufanya hivyo hali hiyo itaendelea kuchangia msongamano magerezani.
Akizungumzia kuhusu Jeshi la Uhamiaji, Kawawa amesema Serikali inapaswa iandae mpango mkakati unaotekelezeka wa kukabiliana na kumaliza wimbi la wahamiaji haramu kutoka nchi mbalimbali hapa nchini.
Pia ameshauri mkakati huo uende sambamba na kutenga bajeti ya kuwarejesha wafungwa wahamiaji haramu waliomaliza kutumikia vifungo vyao.
Awali akiwasilisha makadirio ya wizara yake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Hamad Masauni amesema katika kukabiliana na matukio ya unyang’anyi ambayo yamejitokeza kwa baadhi ya vikundi ya vijana wanajulikana kama Panya Road alitembelea maeneo hayo.
Amesema alipotembelea maeneo hayo alitoa siku saba kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha wanawakamata watu wote waliohusika na matukio hayo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Pia ameagiza kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha wanasambaratisha makundi yote ya wahalifu kabla hayajaleta madhara yoyote kwa wananchi.