Jeshi la Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, linamshikilia kwa mahojiano aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Sweeden, Dk Willibrod Slaa.
Slaa alikamatwa jana usiku nyumbani kwake Mbweni na mpaka sasa Jeshi hilo halijaweka wazi tuhuma zinazomkabili mwanasiasa huyo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ni kwamba tayari wamefanya mahojiano na mwanasiasa huyo na sasa wanaangalia utaratibu wa sheria ili wachukue hatua zaidi.
“Daktari yupo, tuko naye na tumekuwa na mahojiano naye kwa baadhi ya mambo na yanakwenda vizuri kwa hiyo tunaiangalia mifumo ya kisheria inatuelekeza ni nini cha kufanya na taarifa kamili zitatolewa baadaye,” amesema Kamanda Muliro.
Taarifa ya kukamatwa kwa Dk Slaa imesambaa kupitia mitandao ya kijamii, ikisikika sauti ya mwanasiasa huyo akizungumza kuhusu kukamatwa na Jeshi la Polisi na kwamba anapelekwa katika Kituo cha Polisi cha Mbweni, Dar es Salaam.
Hata hivyo kamanda Muliro hakuwa tayari kueleza kwa undani tuhuma zinazomkabili Dk Slaa ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali na viongozi wake.
Dk Slaa aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Mbunge wa Karatu na baadae kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden