, ,

Rais Ruto awashambulia upinzani tena kwa kuondoka kwenye mkutano wa IEBC

Victor Kayanda Avatar

Rais William Ruto ameendelea kuwakosoa viongozi wa upinzani walioondoka kwenye mkutano wa mashauriano na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC), akiwashutumu kwa kupeleka malalamishi yao kuhusu kushindwa kuafikiana kuhusu mgombea mmoja wa urais kwa tume hiyo.

Rais Ruto aliyezungumza akiwa eneo la Funyula, Kaunti ya Busia, wakati wa ziara yake eneo la Magharibi mwa Kenya siku ya Ijumaa, aliwataka viongozi hao kuweka mikakati kuhusu jinsi ya kumpata mgombea wa urais, kuandaa sera na kuwashawishi Wakenya kuunga mkono ajenda yao, badala ya kuingilia maandalizi ya tume hiyo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

“Mliona jana hao watu walienda kugombana na IEBC, wao wameshindwa kutafuta mwaniaji. Badala ya wao kujiuliza maswali wanapeleka kisirani yao kwa IEBC. Kwani wanataka IEBC iwasaidie kutafuta candidate yao? Mimi nataka niwaambie hao majamaa, tafadhalini peeni IEBC nafasi ya kuandaa uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Wakenya watafanya maamuzi yao. Nyinyi endeni kwanza mtafute mgombea wenu, mtafute sera, mtafute ajenda, mtafute mpango, muuzie wananchi tukutane kwa debe. Wachaneni na IEBC.” Alisema Ruto.

Rais pia alihoji wasiwasi wa upinzani kuhusu ununuzi wa vifaa vya kiteknolojia vitakavyotumika katika uchaguzi pamoja na karatasi za kura, akishangaa kwa nini wanasiasa wanataka kuingilia maamuzi ya ununuzi yanayopaswa kufanywa na tume hiyo.

“Ati hao wanataka kuamua ati ni kompyuta gani inafaa kununuliwa. Ati makaratasi itanunuliwa wapi. Kwani hao ni maafisa wa ununuszi? Kwa ile mrengo ilienda pale, iko mtu ako na ujuzi ya ununuzi hapo? Wacheni ufala bwana. Mtu ambaye ni mwaniaji ataamua aje ati kiwanja itakuwa wapi, ati mpira itakuwa gani, ati msimamizi wa mchezo atakuwa nani… Wacheni IEBC. Wenye kura ni wananchi. Kuna msemo wa China unaosema mtu mvivu anagombana na jembe shambani. Analaumu jembe na kumbe yeye ndiye hawezi.” alisema Ruto.

Kauli hizo za Rais zinajiri siku moja tu baada ya viongozi wa upinzani wakiongozwa na kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua, kiongozi wa Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka na Edwin Sifuna wa Linda Mwananchi, miongoni mwa wengine, kuondoka kwenye mkutano wa mashauriano kati ya IEBC na vyama vya kisiasa jijini Nairobi.

Viongozi hao waliishutumu tume hiyo kwa kushindwa kujumuisha masuala muhimu yaliyoibuliwa na Wakenya katika ajenda ya majadiliano kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2027.

Gachagua alisema upinzani ulikuwa umetafuta awali njia rasmi ya kushirikiana na tume hiyo, ikiwemo kupitia jopo la kiufundi lililoongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, lakini akaishutumu IEBC kwa kushindwa kujibu mapendekezo yao.

Upinzani ulisisitiza kuwa majadiliano kuhusu maandalizi ya uchaguzi hayatakuwa na maana iwapo masuala yanayohusu uaminifu, uwazi na uadilifu wa Uchaguzi Mkuu ujao hayatashughulikiwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon alielezea masikitiko yake kuhusu hatua ya viongozi hao kuondoka kwenye mkutano huo, akisisitiza kuwa mkutano huo uliitishwa kuelezea kiwango cha maandalizi ya tume hiyo na kuwapa vyama vya kisiasa fursa ya kujadiliana na tume kuhusu masuala ya uchaguzi.

 

Our Correspondent Avatar