Rushwa yavuruga uchaguzi wa CCM

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefuta matokeo ya uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti Umoja wa Vijana Mkoa wa Simiyu na kusimamisha mchakato wa uchaguzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho katika mikoa ya Mbeya na Arusha.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amewaambia waandishi wa Habari mjini Dodoma leo Novemba 21 kuwa maamuzi hayo yametokana na dosari katika mchakato wa uchaguzi sambamba na tuhuma za rushwa.

Haikufahamika ni lini uchaguzi wa Mwenyekiti UVCCM Simiyu utarudiwa ama maamuzi ya mwisho kuhusu mchakato wa uchaguzi Mkoa wa Mbeya na Arusha yatafanyika.

Kwa mujibu wa Chongolo, leo ni siku ya tatu timu maalumu ya uchunguzi ipo huko ikichunguza zaidi kuhusu kilichojili ili vikao vifanye uamuzi.

Chongolo ametaja sababu kuu ni vitendo vya rushwa ambavyo vimetajwa katika maeneo hayo na kuwa chama hakitavulimia vitendo hivyo pale inapobainika.

“Mbali na hilo, tunachunguza kuhusu uchaguzi wa CCM mkoa wa Mjini Magharibi katika tuhuma za kada mmoja kubeba boksi la kura kwenda nalo chumba cha kuhesabia kura ikibainika tutatoa maelekezo ama ya kufuta matokeo au kuruhusu aliyetangazwa aendelee,” amesema Chongolo.

Kiongozi huyo ambaye ni mkurugenzi wa uchaguzi ndani ya chama amesema hawako tayari kuona viongozi wanaingia madarakani kwa rushwa na vitendo viovu.

Kuhusu adhabu zitakazotolewa alisema ni kuondolewa kwenye mchakato wa uchaguzi na kupelekwa katika vyombo husika.