Search
Close this search box.
Africa

Serikali yatoa sababu za kusitisha zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kieletroniki.

12

Serikali ya Tanzania imesitisha kwa miezi mitatu shughuli ya utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kieletroniki ili kutoa muda wa kufanya tathimini ya kazi hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo.

Majaliwa amesema Serikali imesikia hoja za wafugaji kuhusu mapungufu wa kanuni, usimamizi wake na utekelezaji wake na gharama kubwa ya uwekaji wa hereni za kielektroniki na hivyo kuona kuna haja ya kufanya upya tathmini ya kazi hiyo.

“Serikali imeamua kusitisha utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki kwa kipindi cha miezi mitatu mpaka Januari 31, 2023 wakati ikiendelea na tathmini ambayo itawezesha kutoa mwongozo wa namna bora zaidi ya kutekeleza zoezi hilo kwa mafanikio,”amesema.

Amesema utambuzi kwa hereni ulipaswa kukamilika Oktoba 31,2022 lakini tangu kuanza kwa utekelezaji wa kanuni husika mwaka 2021 hadi kufikia tarehe hiyo idadi ya mifugo iliyowekwa hereni ni milioni tano ambayo imetambuliwa na kusajiliwa sawa na asilimia 11 tu ya lengo la lengo la kutambua mifugo milioni 45.9.

Majaliwa amesema kufuatia hali hiyo Serikali ilitoa taarifa kwa umma kuongeza muda wa utambuzi kwa hiyari Desemba 31, 2022 na baada ya hapo ingechukua hatua za kisheria kwa wasioweka.

Amesema bei elekezi ni ya kutoa huduma hiyo ni shilingi 1,750 kwa ng’ombe na punda,mbuzi na kondoo ni shilingi 1000, gharama ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wafugaji.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema serikali imechukua hatua kadhaa kuboresha sekta ya mifugo kwa kuondoa tozo kadhaa na kutoa ruzuku.

“Serikali imeendelea kutafuta soko la nyama nje ya nchi….tunaendelea kuwasihi wafugaji wafuge kisasa,” amesema Waziri Mkuu.

Sheria ya kufanya utambuzi wa mifugo ilipitishwa mwaka 2010 na kanuni zake zilitungwa 2021.

Comments are closed

Related Posts