Usikilizwaji wa shauri la Kikatiba lililofunguliwa na mawakili Kulwa Maduhu, Nashon Nkung na Paul Kisabo dhidi ya Mamlaka ya Magereza umeendelea leo katika Mahakama Kuu, ambapo shahidi wa nne wa upande wa walalamikiwa alitoa ushahidi na kujibu maswali ya dodoso kutoka kwa mlalamikaji Tundu Lissu.

Katika shauri hilo, mawakili hao wanailalamikia Mamlaka ya Magereza kwa madai ya kuwazuia kuingia katika Gereza Kuu la Ukonga kumwona mteja wao na kutowapatia faragha ya kufanya mazungumzo ya kisheria waliporuhusiwa kuingia gerezani.
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu linaloundwa na Jaji Amir Mruma, Jaji Dkt. Angelo Rumisha na Jaji Dkt. Evaristo Longopa.
Shahidi wa nne, Endrew Shabani Kamanyiro, mwenye umri wa miaka 57 na Mkristo kwa dini, alijitambulisha kuwa Mkuu wa Gereza Kuu la Ukonga. Katika ushahidi wake, alikiri kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kusimamia shughuli zote za gereza hilo na kuwajibika kwa Kamishna Mkuu wa Magereza katika utekelezaji wa sheria, kanuni na usimamizi wa wafungwa.
Katika maswali ya dodoso, Lissu alielekeza hoja zake kwenye mamlaka ya kutunga kanuni za magereza, akimtaka shahidi kufafanua tofauti kati ya Sheria ya Magereza, Kanuni za Magereza na Prison Standing Orders (PSO). Shahidi alikubali kuwa Kanuni za Magereza hutungwa na Waziri mwenye dhamana ya mambo ya ndani, huku PSO zikitungwa na Kamishna Mkuu wa Magereza.
Lissu pia alimuongoza shahidi kupitia vifungu mbalimbali vya Sheria ya Magereza na Kanuni za Magereza vinavyohusu haki za wafungwa kutembelewa na ndugu pamoja na washauri wao wa kisheria. Shahidi alikiri kuwa kanuni zinatambua haki ya wafungwa kutembelewa na mawakili, na kwamba mazungumzo kati ya mfungwa na wakili yanapaswa kuonekana na askari lakini si kusikilizwa.
Katika sehemu nyingine ya dodoso, Lissu alihoji utaratibu unaotumika kwa wafungwa wa adhabu ya kifo, akitaka kufahamu iwapo sheria zinataka mazungumzo yao yasikilizwe na maafisa wa magereza. Shahidi alisisitiza kuwa kanuni hazielezi hivyo.
Maswali mengine yalihusu utaratibu wa ukaguzi wa wageni na nyaraka wanazoingia nazo gerezani. Lissu alirejea Kanuni ya 17 ya Kanuni za Magereza, akidai kuwa ukaguzi unapaswa kufanyika pale tu panapokuwa na sababu ya msingi ya kushuku. Shahidi, kwa upande wake, alieleza kuwa kwa utaratibu wa gereza, kila anayeingia hukaguliwa.
Lissu pia alihoji madai ya kuwepo kwa maafisa wengi wa magereza wakati wa mazungumzo yake na mawakili wake, pamoja na madai ya kuzuiwa kwa baadhi ya viongozi wa CHADEMA kumtembelea. Shahidi alikanusha madai hayo na kusema hajawazuia viongozi hao.
Katika moja ya majibizano yaliyoibua hisia mahakamani, shahidi alisema hawezi kuwaruhusu baadhi ya viongozi waliotajwa na Lissu kumtembelea hadi kesi itakapomalizika.
Kauli hiyo ilipelekea kiongozi wa jopo la majaji watatu Jaji Amiri Mruma, kumuuliza iwapo kulikuwa na amri ya mahakama inayowazuia viongozi hao kutembelea. Shahidi alijibu kuwa hakukuwa na amri ya mahakama, jambo lililosababisha jaji kuendelea kumuhoji kuhusu msingi wa uamuzi huo.
Lissu aliendelea kuhoji iwapo shahidi aliwahi kuwasilisha mahakamani majibu ya kiapo kupinga madai yaliyokuwa yametolewa dhidi yake kuhusu kuwazuia mawakili na viongozi wa kisiasa kumtembelea. Shahidi alikiri kuwa hakuwasilisha kiapo cha kujibu madai hayo.
Kesi imeahirishwa mpaka kesho Julai 23 saa tatu asubuhi ambapo Mawakili wa Serikali watamuuliza Shahidi maswali ya kusawazisha.