Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Shauri la Tozo za Miamala lililofunguliwa na LHRC laondolewa mahakamani - Mwanzo TV

Shauri la Tozo za Miamala lililofunguliwa na LHRC laondolewa mahakamani

Mahakama Kuu ya Tanzania imelazimika kuliondoa mahakamani shauri la maombi ya mapitio ya kimahakama lililofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) la kupinga tozo za miamala ya simu, ili kupisha shauri la rufaa iliyokatwa na upande wa serikali.

Uamuzi huo ulifikiwa mahakamani hapo chini ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji John Mgeta kwa kusaidiana na Jaji Edwin Kakolaki na Jaji Zahra Maruma.

Upande wa serikali walikata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuridhia maombi ya LHRC ya kibali cha kufungua shauri hilo.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Mgeta alisema ni jambo lisilo na ubishi kwamba mara taarifa ya kusudio la kukata rufaa inapowasilishwa katika Mahakama ya Rufani, mamlaka ya Mahakama Kuu katika shauri husika yanakoma.

Alisema maombi hayo ya mapitio ya kimahakama yanatokana na au msingi wake ni uamuzi na amri zilizotolewa na Mahakama Kuu katika shauri namba 11 la 2021, kumpa mwombaji kibali cha kufungua shauri la mapitio ya kimahakama kuhusu tozo hizo.

“Pia haibishaniwi kwamba kwa kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani Oktoba 15, 2021 iliyowasilishwa pia kwa mwombaji (LHRC), wajibu maombi walielezea kusudio lao kupinga uamuzi na amri hiyo, vilevile hakuna ubishi kwamba taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa bado ni halali na kamili kwa kuwa hakuna amri ya Mahakama ya Rufani ambayo imeibatilisha,” alisema.

Alisema kwa mazingira yaliyopo mahakama iliona kutoa kibali cha mapitio ya kimahakama ni uamuzi mdogo usiohitimisha shauri na kwamba kwa kuwa kibali cha kufungua shauri la mapitio ya kimahakama ulitolewa na Mahakama Kuu, haukatiwi rufaa chini ya sheria iliyotumika kufungua maombi hayo ya kibali, hivyo inaweza kuwa hoja ambayo ingeibuliwa na kuamriwa na Mahakama ya Rufani kwenye rufaa inayokusudiwa.

Alisema Desemba 14, mwaka jana mahakama hiyo ilikataa maombi ya upande wa serikali kuomba kibali cha kukata rufaa kupinga uamuzi huo wa kibali cha mapitio ya kimahakama hali iliyofanya upande wa serikali kufungua maombi ya rufaa Mahakama ya Rufani ambayo hayajaamuliwa.

Alisema Mahakama Kuu ina hofu kwamba ikiwa mahakama hiyo itaendelea na usikilizwaji wa shauri hilo na hatimaye ikatoa nafuu zinazoombwa na mwombaji na Mahakama ya Rufani ikaendelea kusikiliza na kuamua rufaa inayokusudiwa kwa manufaa ya wajibu maombi, hiyo inaweza kujenga vurumai katika usimamizi wa utoaji haki na pengine kusababisha mgogoro wa uamuzi au hata kuwaathiri wajibu maombi.

Alisema kwa mazingira hayo mahakama imeona ni vema kutupilia mbali shauri hilo la maombi ya mapitio ya kimahakama ili kutoa njia kwa Mahakama ya Rufani kuona kama rufaa inayokusudiwa inaweza kukubalika.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hili wajibu maombi waliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Erigi Rumisha na mwombaji aliwakilishwa na Wakili Mpale Mpoki.

Wajibu maombi katika shauri hilo ni Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Pamoja na mambo mengine, taasisi hiyo ilikuwa inadai kuwa tozo hizo zimekuwa ni mzigo mkubwa kwa wananchi.