Tanzania kufanya marekebisho ya kodi kila baada ya miaka mitatu

Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa itakuwa inafanya marekebisho ya kodi kila baada ya miaka mitatu ili kuwa na Sera ya kodi inayotabirika na kuwafanya wawekezaji kuweka mipango yenye ufanisi. 

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, wakati wa Kongamano la ukusanyaji maoni ya Kodi Kikanda Jijini Mbeya, ikiwa ni mwendelezo wa makongamano kama hayo yanayofanyika Kanda mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha Sera ya Kodi kwa mwaka 2024/25. 

Alisema kuwa Utaratibu wa sasa ni kufanya marekebisho ya kodi kila baada ya miaka mitatu, hivyo marekebisho yaliyofanywa mwaka huu hayafanyiki tena hadi miaka mitatu ili kuwa na Sera za Kodi inayotabirika. 

“Awali kulikuwa na utratibu ulioasababisha wananchi kusema bajeti ni ya pombe, Sigara na Soda, maana ya kauli hizo ni kuwa kila mwaka Serikali ilikuwa inabadilisha viwango vya kodi vilivyokuwa vinatozwa kwenye bidhaa hizo jambo ambalo kwa sasa halitakuwa linafanyika kila mwaka”, alieleza Bw. Mwandumbya. 

Akizungumzia maboresho ya Kodi yaliyofanyika, Bw. Mwandumbya alisema kuwa Serikali imeongeza bidhaa za mtaji (Capital goods) zinazozalishwa nchini katika wigo wa ahirisho la kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuanzia tarehe Mosi Julai, 2023 na kuondoa katika wigo huo bidhaa za mtaji zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kuanzia tarehe Mosi Julai, 2026.

Alieleza kuwa Nchi imebarikiwa kuwa na watu wengi katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, bidhaa zinazozalishwa katika sekta hizo zinapaswa ziongezwe thamani ili kuwezesha wananchi kupata bei ambazo zitawanufaisha, ili kufanikisha hilo zinahitajika mashine, viwanda vidogo vidogo na vikubwa vitakavyosaidia kuchakata bidhaa hizo kwa maana ya Capital goods.

Alifafanua kuwa Serikali imesamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa utaratibu maalumu kwenye Mashine zinazokwenda kuongeza thamani ya bidhaa ili kuwaongezea wananchi kipato na pia kukuza uchumi wa Taifa. 

Bw. Mwandumbya alisema kuwa ikiwa bidhaa ya mtaji imeingizwa kutoka nje ya nchi ushuru wake umesamehewa, lengo likiwa kuwapeleka wananchi waende kwenye uwekezaji wa viwanda vidogo na vikubwa ili kuongeza thamani ya bidhaa na hatimaye kupata mapato mengi zaidi. 

Pia alisema kuwa Serikali imeweka utaratibu rahisi wa utozaji kodi ya mapato yatokanayo na biashara ya usafirishaji wa abiria, mizigo na utalii kutegemeana na uzito wa gari, idadi ya abiria wanaobebwa, chombo husika pamoja na biashara inayofanywa. 

Alieleza kuwa Gari aina ya Toyota Hiace inayoweza kubeba abiria 18 kodi yake kwa mwaka ni shilingi 550,000 ambayo inalipwa kwa awamu kwa miezi mitatu na Gari aina ya Fuso ya Tani 10 kodi yake ni 750,000 kwa mwaka ambayo pia inalipwa kwa awamu nne. 

Maboresho mengine yaliyofanywa ni kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa vifaa vinavyotumika kubadili mfumo wa magari kutoka matumizi ya mafuta kwenda matumizi ya gesi au umeme na kusamehe kodi hiyo kwenye magari yanayoingia nchini yanayotumia gesi au umeme kwa kuwa nchi inaenda kwenye matumizi ya gesi na umeme kutokana na changamoto kubwa ya mafuta. 

Kwa upande wake, Meneja Huduma wa Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), Bw. Godwin Barongo, alisema kuwa nia ya Utawala bora kwenye mfumo wa kodi nikutaka mlipa kodi alipe kodi ya haki, asionewe lakini pia asiache kulipa kodi halali ya Serikali. 

“Kama kuna mlipa kodi ana malalamiko anayonafasi ya kwenda kwenye Mahakama ya Biashara ambako atakutana na wanasheria, pia anaweza kulalamika kupitia ofisi ya TOST, sisi tutamsikiliza na kuwasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kutatua tatizo ndani ya muda mfupi”, alieleza Bw. Barongo. 

Alisema kuwa Taasisi hiyo haipo kwa ajili ya kuichonganisha Serikali na TRA bali ipo kwa kazi ya kuwasaidia walipa kodi na TRA ili kodi ya Serikali iweze kulipwa kwa uhalali. Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), mkoa wa Mbeya, Bw. Erick Sichinga, alisema kuwa ufafanuzi wa kisheria unaotolewa kupitia Kongamano la ukusanyaji wa Kodi utawasaidia wafanyabiashara kwa kuwa mara nyingi taratibu zinazotumiwa na wafanyabiashara kufikisha maoni Serikalini zilikuwa na mlolongo mrefu hivyo maoni yanafika ikiwa tayari Sheria zimetungwa. 

Bw. Sichinga ameipongeza Wizara ya Fedha kwa uamuzi wa kuwafuata wafanyabiashara katika Kanda zao na kusikiliza maoni yao moja kwa moja na kutoa matumaini ya kufanyiwa kazi kwa kuwa wanauhakika maoni yao yamefika sehemu sahihi na kwa wakati. 

Timu ya Wataalam wa Uchambuzi wa Sera za Kodi kutoka Wizara ya Fedha inaendelea na ukusanyaji wa maoni kwa wananchi Kikanda ambapo hadi sasa mkoa wa Arusha, Mwanza na Kigoma na Mbeya imefikiwa.