Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania (TEC), limetoa waraka wa Kwaresima wa mwaka 2022 ambao kwa sehemu kubwa umejikita kuzungumzia umuhimu wa upatanisho na masuala ya demokrasia nchini humo
Waraka huo wenye kurasa 44, umetolewa na maaskofu wa katoliki 35 ikiwa leo ni Jumatano ya Majivu ambayo ni mwanzo wa kipindi cha Kwaresima, kipindi ambacho madhebu ya kikristo hutumia kipindi hiki kama sehemu pia ya kutubu dhambi zao
Waraka huo, umebeba ujumbe unaosema âTunawasihi kwa jina lake Kristo, Mpatanishwe na Munguâ (2 Kor 5:20).
Katika sura hii, Mtume Paulo ametoa maelezo mbalimbali kumhusu Kristo na mwishoni anahitimisha na kumsihi kila mmoja ajitahidi kupatanishwa na Mungu.
Mwaliko huu ni kiashirio kwamba, maisha ya mkristo lazima yaambatane na jitihada ya kutaka kupatanishwa na Baba wa mbinguni kwa sababu baada ya maisha haya tutarudi kwake.
âMafundisho yote yanayohusu upatanisho ni kipengele muhimu katika mpango wa Mungu wa wokovu. Upatanisho ni neno ambalo mwanadamu hukutana nalo mara nyingi asomapo Maandiko Matakatifu na ndani ya jamii anamoishi. Upatanisho ni sehemu ya wokovu wetu; unakuza mahusiano yetu na Mungu na pia kati yetu,â unaeleza waraka huo
Maaskofu hao wakiongozwa na Gervas Nyaisonga, Askofu Mkuu ambaye pia ni Rais wa Baraza hilo wanasema, upatanisho husaidia watu kuwa huru, kuwajibika, kwa kutetea haki zao na za wengine; kushiriki katika ujenzi wa Taifa kwa umoja, juhudi na maarifa; na kujenga demokrasia kwa kushiriki katika chaguzi zilizo huru na za haki.
Pia katika waraka huo maaskofu hao wanasema, mchakato wa upatanisho husaidia watu kuishi kwa umoja na amani. Lakini uovu hauwezi kuisha kwa kuwa tunaishi katika ulimwengu uliogubikwa na mafarakano; na upatanisho wa kweli ni tumaini la binadamu yeyote anayemwogopa Mungu.
Aidha wamesema Dunia inahitaji kwanza kupatanishwa na Mungu na kisha upatanisho ndani ya jamii. Pasiwepo watu ambao maisha yao yote ni ya manungâuniko sababu tu njia za upatanisho zimefungwa na upande wa pili. Sote tunaalikwa ndani ya jamii ya kitanzania kulitazama na kulifanyia kazi hilo katika ukweli na uadilifu.
âKisiasa, âupatanishoâ wa kweli hupatikana katika kuitafuta, kuiishi na kuilinda demokrasia na amani dumifu,â unaeleza waraka huo na kuongeza:
âIli kufikia demokrasia ya kweli kama njia ya kuelekea mapatano ya kweli, bado yanahitajika majadiliano kati ya wadau mbalimbali wa kisiasa na hasa katika vikao muhimu vya kutoa uamuzi.â
âHivyo basi, viongozi wetu hawana budi kubadilika kuona kwamba demokrasia na utawala bora vinashika hatamu kwa ajili ya manufaa ya wengi.â
Maaskofu hao wanasema, wakati huu wa Kwaresima, kila mmoja katika Taifa la Mungu anahimizwa kutekeleza wajibu wake, kwa njia ya toba, kujenga na kudumisha moyo wa mapatano na uelewano katika jamii.
âHuu ni mwaliko wa kuondokana na ubaguzi wa aina yoyote ile, hususan ubaguzi wa kisiasa. Wakristo hawana budi kuwa ni wadau wa amani ili kudumisha mapatano ya kweli. Haya yote yatawezekana iwapo tu haki, amani, ukweli na uwazi vitatamalaki,â wamesisitiza
Waraka huo unahitimishwa ukisema, âujumbe huu wa Kwaresima kwetu ni mahususi kwa ajili ya ujenzi wa jamii mpya yenye nia ya kuishi kwa umoja na amani kama asemavyo Mzaburi âTazama, jinsi ilivyo vyema, na kupendeza, ndugu wakae pamoja kwa umojaâ (Zab 133:1).
âKukaa huku pamoja haimaanishi kwamba ni kukaa bila tofauti za kimawazo na kimtazamo. La hasha. Bali ni kule kukaa kwa kukubali tofauti hizo bila ya kufarakana,â wanasema
Maaskofu hao wanasema, yumewaandikia ujumbe huu wa Kwaresima kwa Mwaka 2022: âTunawasihi kwa jina lake Kristo, mpatanishwe na Munguâ (2 Kor 5:20), tukitambua kwamba hapa na pale jamii zetu zinafarakana kwa mawazo, kwa maneno, kwa matendo, na kimtazamo.
âNdiyo maana tumesisitiza na tunasisitiza kwamba hayo yanapotokea tunahitaji kupatanishwa. Lengo kuu la upatanisho si kuonekana kwamba mmoja ameshindwa bali ni âkuanza maisha mapya; maisha ya neema.â