Rais William Ruto na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna wameibuka kuwa wagombea wa urais wanaopendelewa zaidi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, huku Sifuna akipendelewa sana miongoni mwa Vijana nchini.
Kwa mujibu wa utafiti mpya uliofanywa na Shirika la TIFA, Rais Ruto na Sifuna wamepokea asilimia 31 ya uungwaji mkono miongoni mwa wakenya waliohojiwa.
Utafiti huo wa mwezi Novemba 2026 unaonyesha kuwa viongozi hao wawili wanawaongoza wagombea wengine walioonyesha ari ya kuwania urais, huku umaarufu wa baadhi ya viongozi wa upinzani ukipungua kadiri umaarufu wa Sifuna unavyozidi kupanda.
Matokeo ya utafiti huo, yaliyotolewa Novemba 12, 2026, yanaonyesha kuwa kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka anafuatia kwa asilimia 9, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i akiwa na asilimia 5, huku aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua akipata asilimia 4.
Mbunge wa Kikuyu Ndindi Nyoro anaungwa mkono na asilimia moja ya waliohojiwa, huku wagombea wengine wakijumuisha asilimia moja. Aidha, asilimia 15 ya waliohojiwa hawajaamua mgombea watakayemuunga mkono, asilimia mbili hawakumpendelea mgombea yeyote, huku asilimia nyingine mbili zikikataa kutoa maoni yao.
TIFA imebainisha kuwa licha ya Ruto na Sifuna kufungamana kwa umaarufu, wagombea wengine wa upinzani kwa pamoja wana uungwaji mkono wa asilimia 19. Kwa mujibu wa kampuni hiyo, idadi hiyo inaweza kumpa Sifuna nafasi ya kufikia kiwango cha asilimia 50 kinachohitajika kushinda urais iwapo vyama vya upinzani vitaungana na kumuunga mkono mgombea mmoja.
Hata hivyo, kampuni hiyo ya utafiti imeonya kuwa ushindi huo hauwezi kuchukuliwa kuwa wa uhakika kutokana na ushindani uliopo miongoni mwa viongozi wa upinzani pamoja na faida zinazotokana na kuwa rais aliye mamlakani.
Utafiti huo umeongeza kuwa iwapo viwango vya sasa vya umaarufu vitasalia bila mabadiliko, nafasi ya Sifuna kuwa mgombea wa pekee wa upinzani inafaa kuzingatiwa.
Ulinganisho wa tafiti zilizopita unaonyesha kuwa uungwaji mkono wa Ruto umeongezeka kutoka asilimia 18 mwezi Agosti 2022 hadi asilimia 31 mwezi Novemba 2026. Kwa upande wake, Sifuna ambaye hakuwa na uungwaji mkono uliorekodiwa katika tafiti za awali, sasa amefikia kiwango sawa na Rais Ruto.
Umaarufu wa Kalonzo umeshuka kutoka asilimia 25 mwezi Novemba 2025 hadi asilimia 9 katika utafiti huo. Uungwaji mkono wa Matiang’i pia umepungua kutoka asilimia 19 hadi asilimia 5 katika kipindi hicho, huku wa Gachagua ukishuka kutoka asilimia 9 mwezi Mei 2026 hadi asilimia 4.
Ndindi Nyoro naye ameanza kujumuishwa katika orodha hiyo akiwa na asilimia moja ya uungwaji mkono. Umaarufu wa wagombea wengine pia umeshuka kutoka asilimia 14 mwezi Septemba 2025 hadi asilimia moja. Idadi ya wale ambao bado hawajaamua imepungua kutoka asilimia 20 mwezi Juni 2026 hadi asilimia 15, huku wale waliokataa kutoa maoni yao wakibaki katika kiwango cha chini cha asilimia 4.
TIFA imeeleza kuwa kupanda kwa umaarufu wa Sifuna kumetokana zaidi na kupungua kwa uungwaji mkono wa wagombea wengine wa upinzani badala ya ule wa Rais Ruto. Kampuni hiyo imeongeza kuwa hakuna mgombea mwingine aliyewahi kuonyesha kiwango kikubwa kama hicho cha uungwaji mkono katika tafiti zinazoangazia wapiga kura kabla ya uchaguzi tangu angalau mwaka 1997.
Utafiti huo pia umeangazia maeneo mbalimbali ya nchi, huku Ruto akirekodi uungwaji mkono mkubwa zaidi katika eneo la Nyanza kwa asilimia 62, akifuatiwa na eneo la Kati kwa asilimia 59 na Pwani kwa asilimia 40. Kwa upande wake, Sifuna ameongoza katika eneo la Magharibi kwa asilimia 55, Nairobi kwa asilimia 39 na Pwani kwa asilimia 36.
Kalonzo anaongoza eneo la Ukambani kwa asilimia 55, huku Matiang’i akipata uungwaji mkono wa asilimia 12 katika eneo la Nyanza Kaskazini. Gachagua naye amepata uungwaji mkono wake mkubwa zaidi katika eneo la Mlima Kenya kwa asilimia 11.
Kwa kuzingatia misimamo ya kisiasa ya wafuasi wa vyama mbalimbali, asilimia 85 ya wafuasi wa UDA wanamuunga mkono Ruto, huku asilimia 90 ya wafuasi wa Linda Mwananchi wakimuunga mkono Sifuna. Miongoni mwa wafuasi wa Wiper, asilimia 80 wanampendelea Kalonzo, huku asilimia 57 ya wafuasi wa Jubilee wakimuunga mkono Matiang’i.
Hata hivyo, miongoni mwa wafuasi wa chama cha DCP kinachoongozwa na Gachagua, Sifuna anaonekana kuwa maarufu zaidi kuliko kiongozi huyo wa chama, akipata asilimia 34 dhidi ya asilimia 25 za Gachagua. Aidha, Sifuna anaungwa mkono na asilimia 33 ya wafuasi wa ODM, ikilinganishwa na asilimia 42 wanaomuunga mkono Ruto.
Utafiti huo pia ulipima athari za serikali jumuishi (Broad-Based Government). Matokeo yanaonyesha kuwa Ruto anaungwa mkono na asilimia 83 ya wanaounga mkono mpangilio huo wa kisiasa, huku Sifuna akipata asilimia 66 ya uungwaji mkono miongoni mwa wanaoupinga.







