, , ,

Uhuru: Wakenya wameamua, shida yao ni umoja wa viongozi wa upinzani

Victor Kayanda Avatar

Rais Mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta amewataka viongozi wa upinzani kuweka kando maslahi na malengo yao ya kibinafsi ya kisiasa na kuungana ili kuwasilisha kwa Wakenya mwelekeo mbadala wa uongozi wa taifa.

Uhuru aliyezungumza wakati wa ibada ya kumbukumbu ya Beatrice Wambui Muturi, ambnaye ni binamuye iliyofanyika katika kanisa la PCEA Nairobi West, eneo la Lang’ata jijini Nairobi, amesema Wakenya wanataka kuona viongozi wanaopinga serikali ya Rais William Ruto wakishirikiana badala ya kuendeleza tofauti zao za kisiasa, akiwataka kujipanga na kutafuta mwafaka kuhusu mustakabali wa kitaifa.

Akizungumzia viongozi hao, akiwemo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, Uhuru amesisitiza kuwa siasa zinahitaji maridhiano na kujitolea, akiwakumbusha kuwa nafasi ya urais hushikiliwa na mtu mmoja pekee kwa wakati mmoja.

“Kama ninavyowaambia ndugu zangu hapa, Steve, Rigathi, Eugene na wengine, mnajua kiti kinaweza kukaliwa na mtu mmoja. Mimi pia nasikiliza yanayojiri mashinani, si kwamba masikio yangu yamezibwa,” alisema Uhuru.

Uhuru amesema mazungumzo yake na wananchi wa kawaida yamemfichulia shauku kubwa ya umma ya kuona viongozi wa upinzani wakiacha tofauti zao na kuungana chini ya ajenda moja.

“Ninapotembea mashinani kutafuta “kauji”, nasikia watu wakisema kwamba wameamua ila tatizo lao ni moja, nalo ni umoja wa viongozi hawa wa upinzani,” akaeleza Uhuru.

Amewataka viongozi hao kuzingatia matakwa ya wananchi na kuchukua hatua za haraka kuimarisha mshikamano wao, akisema Wakenya wanataka kuwaona wakishikana mikono na kuwasilisha mgombea mmoja wa kikosi cha upinzani ili kukabiliana na Rais Ruto debeni mwaka wa 2027.

“Watu wanataka kuwaona viongozi wetu wakishikana. Viongozi wetu, mjipange na muungane ili mtimize kile ambacho Wakenya wanataka,” alisisitiza Uhuru.

Aidha, Uhuru ameelezea matumaini kuwa viongozi hao watazingatia wito wa wananchi na kufanikisha umoja wa kisiasa, akionya kuwa juhudi zozote za kuleta mshikamano nchini lazima ziambatane na haki.

“Na nina hakika hilo ndilo mtakalotufanyia, kwa kuzingatia haki. Hakuwezi kuwa na amani bila haki,” aliongeza.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, pia ametoa wito wa kuimarishwa kwa umoja wa kisiasa, akisema Wakenya wana wajibu wa pamoja wa kukabiliana na changamoto zinazolikabili taifa.

 

Kalonzo amesema huu ndio wakati wa viongozi na wananchi kuweka tofauti zao kando na kuungana katika juhudi za kuokoa mustakabali wa nchi.

“Wakati umefika kwa sisi sote kuokoa taifa letu,” alisema Kalonzo.

Aidha, ametetea haki ya vijana kujieleza kisiasa, akipinga vikali matamshi yanayoagiza maafisa wa polisi kuwapiga risasi miguuni waandamanaji.

Akizungumzia matamshi ya kuwataka vijana wa Gen Z kupigwa risasi miguuni, Kalonzo alisema kauli hiyo inaashiria hofu ya uongozi wa urais, akidai kuwa ndiyo sababu Wakenya wanaendelea kutoa wito wa kutaka Rais Ruto ahudumu muhula mmoja pekee.

“Mtu anaposema, ‘Wapigeni Gen Z risasi miguuni,’ hiyo ni hofu ya urais. Na hii ndiyo sababu Wakenya wameungana kutoa wito wa kutaka muhula mmoja pekee,” alisema Kalonzo.

Naye Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amekiri kuwa jamii ya Mlima Kenya ilipuuza ushauri wa Kenyatta dhidi ya kumchagua William Ruto katika uchaguzi mkuu uliopita, akisema eneo hilo sasa linajutia uamuzi huo.

Gachagua alisema Uhuru alikuwa amewaonya wakazi wa Mlima Kenya dhidi ya kumuunga mkono Ruto katika kinyang’anyiro cha urais, lakini hawakuzingatia ushauri huo.

Gachagua alisema badala yake, jamii hiyo iliungana kumuunga mkono Ruto, uamuzi ambao sasa anasema wameujutia, akiongeza kuwa hata yeye binafsi alikumbwa na madhara ya kisiasa baada ya kuzozana na Rais huyo.

“Baba Ngina alituita na kutuambia tusimchague mtu huyu, lakini tulikataa kusikiliza. Tulimchagua, na ndiyo maana tuko hapa leo. Hata mimi sikuachwa; nilifurushwa na kwenda Wamunyoro, lakini Mungu ni mwema, sikufa,” alisema Gachagua.

Matamshi ya Gachagua yanaashiria kukiri kwake hadharani kuwa jamii ya Mlima Kenya ilifanya uamuzi wa kisiasa kinyume na msimamo wa Uhuru katika uchaguzi wa 2022, huku uhusiano wake na Rais Ruto ukivunjika na kusababisha kuondolewa kwake mamlakani kupitia mchakato wa kumwondoa madarakani mwaka 2024.

 

 

 

Our Correspondent Avatar