UN yaitaka Tanzania kuchukua hatua za haraka kukabiliana na ukiukwaji wa haki za binadamu kabla ya uchaguzi

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameitaka Tanzania kuacha kuendelea na ongezeko la ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wanachama wa vyama vya upinzani, mashirika ya kiraia, waandishi wa habari, watu wa asili na watoa huduma za haki za binadamu.

Katika kuelekea uchaguzi wa mitaa mwezi Novemba 2024 na uchaguzi wa rais mwezi Oktoba 2025, usajili wa wapiga kura na mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani umekumbwa na unyanyasaji na vitisho, kukamatwa kiholela, kunyimwa uhuru, utekaji nyara, mateso, mauaji yasiyo ya kisheria na vizuizi dhidi ya uhuru wa kutoa maoni.

“Tuna hofu juu ya kuongezeka kwa matukio ya kutekwa na kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji yaliyorekodiwa ya waandamanaji na wanachama wa vyama vya upinzani. Tuna wasiwasi kwamba mtindo huu wa ukandamizaji unalenga kuzuia upinzani wa kisiasa na kutisha upinzani kwa Serikali, na utaathiri mchakato wa kidemokrasia na uchaguzi wa kitaifa,” walisema wataalamu hao.

“Tuna wasiwasi pia kuhusu vizuizi vilivyoripotiwa dhidi ya upatikanaji wa baadhi ya mitandao ya kijamii na kusimamishwa kwa leseni za waandishi wa habari katika kulipiza kisasi kwa kusambaza video ya utetezi wa haki za binadamu, na tunawaomba Serikali kurejesha mara moja,” walisema.

Serikali ya Tanzania inaripotiwa kutumia Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kufuta usajili wa kiholela na kuweka vikwazo kwa shughuli za mashirika ya kiraia. Aidha, tarehe 2 Agosti 2024, kupitia uamuzi wa Serikali (Tangazo Na. 673), mamlaka zilifuta usajili wa vijiji kadhaa ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Vitendo hivi vya kuhamasisha usajili wa wananchi wa Msomera – eneo lililo takribani kilomita 600 bila  ridhaa ya wananchi, vilisababisha wasiwasi mkubwa na kusababisha maandamano ya amani miongoni mwa Wamasai wa asili, ambao waliona hatua hii kama tishio moja kwa moja kwa ardhi na maisha yao ya jadi.

Wataalamu hao walipongeza uamuzi wa Mahakama Kuu ya Arusha wa tarehe 22 Agosti 2024 wa kusitisha kwa muda Tangazo Na. 673 na uamuzi uliofuata uliojadiliwa katika Matangazo 796 na 797 ya Septemba 2024, ukirejesha maeneo ya kiutawala, ikiwa ni pamoja na sehemu za Wilaya ya Ngorongoro.

“Tunaona kuwa Serikali imechukua hatua halisi za kubadili uamuzi wa kufuta usajili wa vijiji kadhaa ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kurejesha haki zao za kisiasa na umma, ambayo ni muhimu kwa kukuza utawala wa kidemokrasia, ujumuishwaji wa kijamii na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu kwa Watu wa Asili. Tunaiomba Serikali kuhakikisha kuwa inatekeleza kikamilifu uamuzi huo na kuhakikisha kuwa wakazi wote wa vijiji wanapewa uhuru wa kujisajili katika vijiji vyao,” walisema.

“Tunaunga mkono mazungumzo zaidi yenye maana na Wamasai, ikiwa ni pamoja na viongozi wao, kama muhimu katika kutafuta suluhu endelevu inayoheshimu haki za ardhi, maeneo na rasilimali za Wamasai wa asili,” walisema wataalamu hao na kuongeza

Aidha wameitaka Tanzania kushughulikia suala la utekaji na ukiukwaji mwingine wa Haki za Binadamu uliofanywa katika muktadha wa uchaguzi si tu kuhusu kujibu matukio baada ya kutokea, bali pia ni kuunda mazingira ambapo sauti nyingi zinatolewa, ikiwa ni pamoja na vyama vya upinzani na vikundi vilivyotengwa, kuzuia ukosefu wa uwajibikaji na kuheshimu utawala wa sheria.

Pamoja nahayo wamesisitiza kwamba wataendelea kujihusisha na mamlaka nchini Tanzania na kufuatilia kwa karibu hali hiyo kuhakikisha kwamba matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu hayaendelei.