Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, linasema watoto na familia zao katika pembe ya Afrika wamekata tamaa na maisha yao yako ukingoni.
Mkurugenzi wa UNICEF wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Mohamed M Fall amesema, mahitaji ni makubwa na ya dharura, na yanavuka kwa haraka fedha zilizopo ili kukabiliana na hali hiyo.
“Tunahitaji kuchukua hatua sasa ili kuzuia maafa. UNICEF inakadiria kuwa hadi watu milioni 20 katika Eritrea, Ethiopia, Kenya na Somalia watahitaji maji na chakula katika muda wa miezi sita ijayo. Hiyo ni karibu idadi sawa ya watu wa Ugiriki na Uswidi kwa pamoja.”
Bwana Fall amasema wengi wao ni watoto, ambao wako katika hatari kubwa zaidi kutokana na moja ya dharura mbaya zaidi iliyosababishwa na tabianchi katika kipindi cha miaka 40 iliyopita na kwamba kanda hii haiwezi kustahimili dhoruba nyingine kamilifu, ikichanganya na ugonjwa wa COVID-19, migogoro na mabadiliko ya tabianchi.
“Na bado, tuko hapa. Na ni watoto ambao wanalipa gharama kubwa zaidi kwa majanga ambayo hawakusababisha. Misimu mitatu ya kiangazi mfululizo imesababisha uhaba mkubwa wa maji, kuua mifugo na mazao, kuhamisha watu, na kuongeza hatari ya magonjwa na utapiamlo mkali.” -Anasema Bwana Fall
Na kuongeza kuwa, “hivi sasa, takribani watoto milioni 5.5 katika nchi hizi nne wanatishiwa na utapiamlo mkali na inakadiriwa watoto milioni 1.4 wana utapiamlo mkali”
UNICEF inahofia kwamba idadi hii itaongezeka kwa asilimia 50 ikiwa mvua hazitanyesha katika miezi mitatu ijayo. Somalia pekee, inakadiriwa kuwa watoto milioni 1.3 chini ya umri wa miaka 5 ambao wako katika hatari ya utapiamlo, ikiwa ni pamoja na karibu watoto 295,000 ambao wako katika hali mbaya.
Ombi la UNICEF sasa ni dola za Marekani milioni 123 kwa nchi hizi nne pekee ili kushughulikia mahitaji ya kuokoa maisha kwa walio hatarini zaidi hadi mwisho wa Juni 2022, ili kuzuia maafa kwa watoto na familia zao.