Viongozi wa upinzani wamemkashifu Rais William Ruto kwa kile walichokitaja kuwa jaribio la kunyakua mradi wa Soko la Masinde Muliro mjini Kitale kaunti ya Trans Nzoia huku mzozo kuhusu aliyehusika na ujenzi wa soko hilo ukiendelea kutokota kati yake na Gavana George Natembeya.
Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka alisema hatua ya Rais kuhusishwa na mradi huo inaashiria kile alichodai kuwa ni kushindwa kwa serikali ya kitaifa kutekeleza miradi ya maendeleo na sasa inajaribu kujipatia umaarufu wa kisiasa kupitia mradi inayotekelezwa na serikali za kaunti.
Kalonzo alisema Rais Ruto anafanya hivyo kwa kutoa vitisho kama vile kuwapokofanya walinzi viongozi wasiounga mkono serikali yake na kuwaelekezea cheche za maneno kila mara.
“Gavana Natembeya ambaye anawindwa na Rais Ruto. Isije ikadhaniwa kuwa ni suala la kaunti ya Trans Nzoia. Kudhulumiwa kwa Gavana Natembeya ni suala la kitaifa. Gavana aliyechaguliwa na wenyeji wa kaunti alishambuliwa kwa vitoa machozi baada yake kukutana na msafara wa Rais Ruto katika kaunti yake siku ya Ijumaa. Ni jambo la kusikitisha mno,” Kalonzo alisema.
Vuguvugu la Linda Mwananchi kwa upande wake limeunga mkono msimamo wa Gavana Natembeya kwamba serikali ya kaunti ndiyo iliyotekeleza mradi huo, likimtaka Rais Ruto kuheshimu mamlaka ya serikali za ugatuzi na kujiepusha na tamaa ya kujipatia sifa kwa miradi ambayo haiko chini ya mamlaka ya serikali yake.
Katika taarifa yake, vuguvugu hilo limedai kuwa Rais Ruto anahofia muda wa muhula wake kuisha bila kuwa na mafanikio ya kutosha ya kujivunia, likisema Wakenya watapata fursa ya kumwondoa mamlakani kupitia uchaguzi wa mwaka wa 2027.
Vuguvugu hilo pia limeutaja mzozo wa soko la Kitale kuwa sehemu ya mapambano ya kulinda ugatuzi na Katiba dhidi ya juhudi za kudhoofisha mamlaka ya serikali za kaunti.
Kwa mujibu wa Linda Mwananchi, ujenzi wa masoko ni mojawapo ya majukumu ya serikali za kaunti, kama ilivyoainishwa katika Sehemu ya Pili, aya ya saba ya Katiba ya Kenya, inayozipa kaunti jukumu la kusimamia maendeleo na udhibiti wa biashara, ikiwemo masoko.
Vuguvugu hilo limesema mradi wa Soko la Masinde Muliro ulianzishwa na Serikali ya Kaunti ya Trans Nzoia mwaka wa kifedha wa 2017/2018 kwa gharama iliyokadiriwa kuwa shilingi milioni 874.28.
Hata hivyo, mradi huo ulikumbwa na maswali ya ukaguzi kutoka kwa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu kuchelewa kukamilika kwake na kuongezwa kwa muda wa utekelezaji, hali iliyosababisha mabadiliko ya gharama za mradi.
Linda Mwananchi imesema Gavana Natembeya alipoingia mamlakani alikuta masuala hayo yakiendelea kushughulikiwa, na baadaye akaelekezwa na Kamati ya Seneti ya Uwekezaji wa Umma katika Kaunti kuyatatua, hatua ambayo vuguvugu hilo limesema ilitekelezwa.
Katika ujumbe wake, vuguvugu hilo limetoa wito kwa Wakenya kuungana katika kulinda ugatuzi, likilinganisha mapambano hayo na juhudi za mashujaa wa uhuru waliopigania kuikomboa nchi dhidi ya ukoloni na udikteta.
Wakati uo huo, Gavana Natembeya amesema hataogopa wala kutishwa na vitisho dhidi ya usalama wake, kufuatia kuondolewa kwa maafisa wa usalama waliokuwa wakimlinda.
Mzozo huo unaendelea kuibua mjadala kuhusu mipaka ya majukumu ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti, pamoja na namna miradi ya maendeleo inavyopaswa kutekelezwa na kutambuliwa chini ya mfumo wa ugatuzi.








