Wahamiaji haramu 78, raia wa Ethiopia wakamatwa

Jeshi la Uhamiaji Mkoani Iringa kwa kushirikiana na ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa limekamata wahamiaji haramu 78 raia wa Ethiopia na Watanzania wawili.

Akitoa taarifa hiyo leo, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji Mkoani Iringa, Agnes Luziga amesema raia hao wamekamatwa jana March 8, 2022 majira ya saa moja jioni.

Luziga amesema kuwa wahamiaji hao wamekamatwa katika eneo la Kihesa Kilolo lililopo ndani ya Manispaa ya Iringa wakisafirishwa kwa kutumia lori.

Ameeleza kuwa jana jioni alipata taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa kuna gari linasadikiwa kubeba wahamiaji haramu ambalo katika gari hilo kulikuwa na stika ya TRA halisi ambayo ilikuwa sio rahisi kwa mtu kugundua.

Amesema baada ya kukamata gari hilo, walishirikiana na TRA kulikagua gari na kulifungua na kutokana na stika hiyo wahamiaji hao waliingia ndani ya gari kwa kupitia matundu yaliyokuwa yametobolewa juu ya gari hiyo.

“Wahamiaji tuliowakamata ni raia wa Ethiopia wametokea Ethiopia kupitia mpaka wa Hororo-Taveta wakielekea Nchini Afrika Kusini wakienda kutafuta maisha hivyo taratibu za kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hawa zinaendelea,” amesema.

Luziga amewataka wananchi pindi wanapopata taarifa kuhusu wahamiaji haramu watoe taarifa katika ofisi za uhamiaji ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Mmoja wa wanaodaiwa kusafirisha wahamiaji hao, Daniel Dutamo amesema yeye hupokea raia hao na kuwasafirisha kutoka maeneo tofauti na hupewa pesa, huku akidai kuwa hawajala chakula tangu walivyokamatwa.

“Mpaka leo tayari tumetumia miezi miwili na hatukuwa na chakula isipokuwa kwenye gari tulikuwa na maji mengi.

“Tangu tukamatwe hapa Iringa hatujala chakula chochote hivyo tunaomba angalau watupe chakula kwa sababu wengine afya zao sio nzuri kutokana na kukaa njaa muda mrefu,” amesema.