
Kituo hicho kinajengwa katika Kambi ya Anga ya Laikipia, iliyopo Nanyuki chini ya Mlima Kenya, na kinatarajiwa kutumika kuwaweka karantini raia wa Marekani watakaowasili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambayo kwa sasa inakabiliwa na mlipuko mkubwa wa ugonjwa wa Ebola.
Kenya haijawahi kurekodi kisa chochote cha Ebola, jambo ambalo limewafanya wananchi wengi kupinga mpango wa kuwaruhusu watu wanaoweza kuwa wabebaji wa ugonjwa huo hatari kuingia nchini.
Makumi ya waandamanaji walikusanyika karibu na kambi hiyo ya anga, huku baadhi yao wakivaa vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi na kubeba jeneza lililoandikwa neno “Ebola”.
Kituo hicho kinatarajiwa kuwa na vitanda 50 vya wagonjwa waliowekwa karantini na kusimamiwa na wafanyakazi kutoka Marekani. Ujenzi wake ulikuwa ukikaribia kukamilika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Tayari mradi huo ulizua maandamano mnamo Juni 1. Makundi ya kutetea haki za binadamu yalisema watu wawili walifariki dunia wakati wa maandamano hayo, ingawa mazingira ya vifo vyao bado hayajabainika.
Ujenzi wa kituo hicho kwa sasa umesitishwa kwa amri ya muda ya Mahakama Kuu ya Kenya, huku ukipingwa pia na baadhi ya viongozi wa kisiasa wa Kaunti ya Laikipia.
Hata hivyo, Serikali ya Rais William Ruto imeapa kuendelea na mradi huo, ikisema Kenya ina wajibu wa kushirikiana na Marekani kutokana na msaada mkubwa ambao imekuwa ikipokea kwa miaka mingi.
“Wananchi na Serikali ya Marekani wamekuwa washirika wetu katika masuala ya afya kwa takribani miaka 25 hadi 30,” alisema Rais Ruto wiki iliyopita.
“Lingekuwa jambo la kusikitisha sana kama tungekataa ombi moja la Marekani la kujenga kituo kwa gharama zao wenyewe. Hilo lingeonekana kutokuwa na ubinadamu.”
Waziri wa Afya wa Kenya pia amesisitiza kuwa kituo hicho hakitawanufaisha Wamarekani pekee bali pia Wakenya.
Marekani imeahidi kutoa dola milioni 13.5 kusaidia juhudi za Kenya za kujiandaa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.
Hatua hiyo inafuatia makubaliano ya kiafya yaliyoibua mjadala mwaka jana, ambapo Kenya ilikubali kushirikisha Marekani kiasi kikubwa cha takwimu za afya kwa kubadilishana na msaada wa mabilioni ya dola.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza mlipuko wa Ebola nchini DRC kuwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa, baada ya kuthibitishwa kwa maambukizi 515 na vifo 91.
Licha ya hofu ya ugonjwa huo kusambaa katika nchi jirani, ni Uganda pekee ambayo imeripoti visa vya Ebola hadi sasa. Nchi hiyo imethibitisha visa 19, ambapo wengi wa waathirika ni raia wa Congo waliovuka mpaka kuingia Uganda.