Wanafunzi wa Watanzania wafanikiwa kuondoka Ukraine

Kundi la mwisho la wanafunzi 32 wa Tanzania waliokuwa wamekwama katika mji wa Sumy limefanikiwa kuondoka kuelekea katika miji ya Poltavo na Lviv nchini Ukraine na kuingia katika nchi za Hungary na Poland.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano Serikalini, Emmanuel Buhohela imesema kwa sasa hakuna mwanafunzi kutoka Tanzania aliyebaki kwenye Chuo cha Taifa cha Sumy kilichopo nchini Ukraine baada ya kundi hilo la mwisho kufanikiwa kuondoka.

Kundi hilo limefanikiwa baada ya mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Tanzania, Balozi Liberata Mulamula na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba.

“Hatua hiyo imefikiwa baada ya mazungurnzo yaliyofanyika kwa njia ya simu kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba Machi 07, 2022 kwa lengo la kuiomba Serikali ya Ukraine kusaidia kuwatoa Watanzania wanaosoma katika Chuo cha Sumy” imesema taarifa hiyo na kuongeza:

Katika Mazungumzo hayo, Naibu Waziri Kuleba aliridhia ombi la kuwasaidia wanafunzi hao kuondoka nchini Ukraine salama kupitia mipaka ya Poland na Hungary kwa utaratibu ulioratibiwa na Balozi za Tanzania nchini Sweden, Ujeruman pamoja na Urusi na kusimamiwa na uongozi wa Chuo cha Sumy.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanafunzi wengine 61 waliondoka katika chuo cha Sumy Machi 08, 2022 alfajiri ambapo kati yao 50 wanatarajiwa kuingia nchini Hungary na 11 nchini Poland.

Pia, taarifa hiyo imesema kuwa maofisa wa Balozi za Tanzania nchini Sweden na Ujerumani wako tayari kwenye mipaka ya Poland kwenda Hungary kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi hao.

Serikati kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawashukuru kwa dhati Watanzania (Diaspora) wanaoishi Ukraine, Poland, Romania na Hungary, pia Mkurugenzi wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel na kamati ya wazazi wa wanafunzi kwa utulivu wao na kuisaidia Serikali kutekeleza wajibu wake bila shinikizo na kufanikiwa kuwaondoa Watanzania wote nchini Ukraine wakiwa salama.” imesema  taarifa hiyo