Wanasiasa na Wanaharakati waishambulia Ofisi ya Msajili kwa kutishia kuifuta Chadema

Wanasiasa, wanaharakati na wasomi wa sheria nchini Tanzania wameendelea kuikosoa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufuatia hatua yake ya kukitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujieleza ndani ya siku 13 kwa nini kisichukuliwe hatua za kisheria, ikiwemo kusimamishiwa usajili au kutozwa faini.

Ukosoaji huo umeongezeka katika mtandao wa X, ambapo viongozi mbalimbali wa kisiasa, wanasheria na watetezi wa haki za binadamu wameeleza wasiwasi wao kuhusu kile wanachodai kuwa ni matumizi ya mamlaka yanayoweza kuhatarisha demokrasia na ushindani wa kisiasa nchini.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, ni miongoni mwa waliotoa kauli kali zaidi dhidi ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Kupitia ukurasa wake wa X, Mwabukusi alisema ofisi hiyo imekuwa “chemchemi ya vurugu za kidemokrasia” ndani ya vyama vya upinzani na kuhusishwa moja kwa moja na mazingira yaliyopelekea vurugu na mauaji ya Oktoba 29, 2025.

Mwabukusi alidai kuwa baadhi ya maofisa wa ofisi hiyo wanatumia mamlaka vibaya kwa misingi ya ubaguzi, upendeleo na kile alichokiita “kujipendekeza kisiasa,” hali ambayo amesema inachochea migogoro ya kisiasa badala ya kuisimamia kwa haki.

“Tunaweza kulaumu Polisi, Mahakama na vyombo vingine vya dola, lakini tusisahau kuwa kinu kinachoandaa hila na machafuko ni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,” aliandika Mwabukusi.

Kauli hiyo imeungwa mkono na baadhi ya wachambuzi wa siasa na wanaharakati wa haki za kiraia waliotumia mitandao ya kijamii kueleza kuwa hatua dhidi ya Chadema zinaweza kuongeza mvutano wa kisiasa nchini, hasa katika kipindi ambacho taifa linaendelea kujadili mustakabali wa mageuzi ya uchaguzi na uhuru wa kisiasa.

Naye kiongozi wa zamani wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameonya dhidi ya kile alichokiita “jaribio la kuifuta Chadema kisiasa.”

Katika ujumbe wake aliouchapisha kwenye X, Zitto alisema “tishio lolote dhidi ya Chadema ni tishio dhidi ya demokrasia,” huku akiitaka Ofisi ya Msajili kusitisha hatua hizo mara moja.

“Zama za Ofisi ya Msajili kuwa mchezaji namba 12 wa CCM zimekwisha,” aliandika Zitto, akiongeza kuwa taasisi za dola zinapaswa kuviacha vyama vya siasa kushindana kisiasa bila kuingiliwa.

Mwanasiasa huyo pia alihoji kile alichodai kuwa ni ukosefu wa usawa katika utekelezaji wa sheria za vyama vya siasa, akisema kuna madai mengi dhidi ya chama tawala CCM ambayo hayajawahi kuchukuliwa hatua na Msajili wa Vyama.

Kauli hizo zimekuja baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuitaka Chadema kujieleza kufuatia matamko mbalimbali yaliyotolewa na viongozi wake katika nyakati tofauti, ambayo ofisi hiyo inadai yanaweza kuchochea vurugu.

Kwa mujibu wa barua yenye kumbukumbu namba HA.322/362/16A/22 ya Mei 7, 2026, iliyosainiwa na Kaimu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, ofisi hiyo imeeleza kuwa imebaini ukiukwaji wa masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa kupitia kauli za viongozi wa Chadema pamoja na maazimio yaliyotolewa na Kamati Kuu ya chama hicho mwishoni mwa Aprili mwaka huu.

Miongoni mwa matukio yaliyotajwa ni kauli za Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, kuhusu maandamano ya nchi nzima ya kushinikiza kuachiwa kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi mahakamani.

Akizungumza Mei 13 nje ya Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alithibitisha chama hicho kupokea barua hiyo lakini hakutaka kuweka wazi maudhui yake akisema bado wanaendelea kuifanyia kazi.

Hatua hiyo ya Msajili imekuja pia katika kipindi ambacho Chadema imekuwa katika mvutano wa muda mrefu na ofisi hiyo kuhusu uhalali wa baadhi ya uteuzi wa viongozi wake wa juu pamoja na masuala ya ruzuku ya chama. Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanaonya kuwa mvutano huo unaweza kuongeza hali ya kutokuaminiana kati ya vyama vya upinzani na taasisi za dola ikiwa hakutakuwa na juhudi za kujenga mazingira ya ushindani wa kisiasa yanayoonekana kuwa ya haki kwa pande zote.

Wakati mjadala huo ukiendelea, macho ya wengi sasa yanaelekezwa kwa Chadema kuona itakavyotoa majibu yake kwa Ofisi ya Msajili, pamoja na hatua ambazo mamlaka zitachukua baada ya muda wa siku 13 uliotolewa kumalizika.