Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi imewatia hatiani washtakiwa wanne katika kesi ya uhujumu uchumi namba 2 ya mwaka 2022 inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na kuwataka kulipa fidia ya shilingi milioni moja kila mmoja pamoja na faini ya shilingi elfu 50 kila mmoja kwa kila kosa ambapo wanakabiliwa na makosa mawili.
Agosti 3 mwaka huu washtakiwa wanne waliokuwa katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Sabaya ambao ni Silvester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey waliandika barua ya kuomba kufanya makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuhusu shauri linalowakabili.
Awali akiwasilisha ombi la kuombwa kuondolewa mashtaka washtakiwa hao wanne, Mkurugenzi Msaidizi wa Kurugenzi ya kutenganisha upelelezi na mashtaka wa ofisi ya DPP, Martenus Marandu alidai mahakamani hapo kuwa ofisi yake imekubali kuingia makubaliano na washtakiwa hao.
Mkurugenzi Msaidizi Marandu ameendelea kudai kuwa washtakiwa kwa pamoja wamekubali kufanya makubaliano kwa mujibu wa sheria, ili kufutiwa mashtaka yanayowakabili.
Kutokana na makubaliano hayo, kwa mujibu wa sheria washtakiwa wamesomewa upya mashataka yao na kukiri kosa ambapo mahakama baada ya kuwahoji kama wana pingamizi, washtakiwa hao walisema hawana na hivyo mahakama ikawatia hatiani kwa makossa mawili ya kujitwalia mamlaka ya kufanya upekuzi nyumbani kwa Alex Swai mkazi wa kijiji cha Mbosho wilayani Hai pamoja na kula njama kushinda utaratibu wa haki.
Akitoa uamuzi baada ya washtakiwa kukiri makosa, hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi Salome Mshasha amesema, washtakiwa hao wamekubali wenyewe kuingia makubaliano na upande wa Jamhuri na wamekiri makosa kwa mashtaka ambayo wanakubaliana nayo.
Hakimu Mkazi Mwandamizi Mshasha amesema amezingatia makubaliano ya upande wa mashtaka na washtakiwa pamoja na maelezo ambayo yametolewa mbele ya mahakama.
Kwa mujibu wa kifungu namba 194 D kifungu kidogo cha sita cha sheria ya makosa ya jinai sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo na sheria ya mwaka 2022 ambacho kinaelekeza iwapo washtakiwa watatiwa hatiani kwa kosa wanaloshtakiwa baada ya kupunguziwa makosa, adhabu itakayotolewa itatolewa kupitia msingi wa makubaliano.
Washtakiwa hao wamelipa faini na wameachiwa huru.