Search
Close this search box.
Africa
Chanjo dhidi ya homa ya Ini aina ya B Argentina

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO, linaendelea kufutiatilia ripoti za kubainika kwa ugonjwa wa homa ya ini, Hepatitism miongoni mwa watoto, ingawa hadi sasa halijafahamu ni aina gani ya homa ya ini. 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo jana akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi, mkutano ambao huwa mahsusi kwa ajili ya kutoa ripoti kuhusu mwelekeo wa ugonjwa wa Corona taarifa nyingine. 

“WHO imepokea ripoti za zaidi ya watoto 700 wanaoshukiwa kuwa na homa ya ini katika nchi 34 na wagonjwa wengine 112 wanachunguzwa,” amesema Dkt. Tedros. 

Kwa sasa takribani watoto 38 kati ya hao 700 wanahitaji kupandikizwa ini na 10 wamefariki dunia. 

WHO inaendelea kushirikiana na nchi ambamo wagonjwa hao wamebainika ili kuchunguza sababu ya kuwepo kwa ugonjwa huo wa ini kwa watoto hao. 

Cha kustaajabisha hadi sasa aina 5 za virusi ambavyo hutambuliwa kusababisha homa ya ini havijagundulika miongoni mwa watoto hao. 

Kila mwaka, WHO hupokea taarifa za watoto kuwa na ugonjwa wa homa ya ini usioendana na aina za virusi vinavyotambulika, lakini baadhi ya nchi zimedokeza kuwa idadi ya watoto wanaogundulika ni kubwa kuliko ile iliyotarajiwa. 

COVID-19 maambukizi na vifo imepungua 

Akizungumzia COVID-19, Dkt. Tedros amesema idadi ya wagonjwa wapya na vifo imepungua, “huu ni mwelekeo unaotia matumaini ya kwamba ongezeko la utoaji chanjo linaokoa maisha lakini bado tunaendelea kutoa tahadhari.” 

Amesema ingawa chanjo zipo, bado mahitaji katika baadhi ya nchi yamepungua, halikadhalika utoaji wa chanjo. 

“WHO na wadau tunaendelea kushirikiana na serikali kuongeza kasi ya utoaji wa chanjo kwa kuzipeleka pale watu waliko, kupitia mlango kwa mlango, gari kwa gari na kuhamaisha viongozi wa kijamii,” amesema Dkt. Tedros. 

Fikra ya kwamba janga limeisha inaeleweka lakini haiko sawa. 

Aina mpya ya virusi inaweza kuibuka wakati wowote na watu wengi hawajapatiwa chanjo, “janga halijaisha, na tutaendelea kusema hivi hadi litokomee.”

Kadhalika Dkt. Tedros, amezungumzia hali ya ugongwa wa Monkeypox ambapo amesema zaidi ya watu 1,000 wamethibishwa kuugua ugonjwa wa Monkeypox katika nchi 29 ambazo hazijazoea kuwa na ugonjwa huo lakini hakuna kifo. 

Maambukizi sasa siyo tu kwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao bali pia yamebainika miongoni mwa wanajamii wakiwemo wanawake. 

WHO imetoa mwongozo kwa nchi wa kuwezesha kufuatilia wagonjwa, kusimamia na uchunguzi. 

“Siku zijazo, tutatoa mwongozo wa tiba,  udhibiti wa maambukizi na chanjo,” amesema Dkt. Tedros.

Comments are closed