Mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2026/2027 umechukua sura mpya baada ya Mbunge wa Jimbo la Tunguu, Zanzibar, Simai Mohammed Said, kutoa kauli kali dhidi ya kile alichodai kuwa ni usaliti unaofanywa na mmoja wa viongozi waliopo ndani ya Serikali.
Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha bungeni, mbunge huyo alisema Serikali inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhimiza mshikamano, upendo na maendeleo ya taifa, lakini mafanikio hayo yanakwamishwa na baadhi ya watu wanaokwenda kinyume na matarajio ya uongozi.
“Rais Samia ameiongoza Serikali yake kwa upendo na mshikamano, lakini wakati mwingine mafanikio yetu yanakumbana na watu wanaotutendea kinyume,” alisema.
Katika kauli yake iliyovuta hisia za wabunge na wananchi wanaofuatilia mijadala ya Bunge, Simai alimtaja mtu huyo kwa jina la mfano la “Yuda”, akimaanisha mhusika anayesaliti wale aliokuwa akishirikiana nao kisiasa.
“Binadamu ni walewale. Lakini leo namwita mmoja aliyepo ndani ya Serikali kwa jina la Yuda. Tunataka maendeleo ya nchi yetu. Kosa la Mama ni lipi hadi mtu aliyemuamini ageuke kuwa msaliti?” alihoji.
Mbunge huyo aliendelea kudai kuwa mtu anayemlenga si tu kwamba amewasaliti wenzake, bali pia amepoteza uungwaji mkono kutoka kwa watu waliowahi kuwa karibu naye kisiasa.
Kwa mujibu wa Simai, mhusika huyo amekuwa chanzo cha misukosuko ya kisiasa inayowagusa baadhi ya watendaji na viongozi, hali ambayo amesema imeathiri hata utendaji wa baadhi ya watu ndani ya mfumo wa Serikali na chama.
Alidai pia kuwa katika siku za karibuni, mtu huyo ameonekana katika nyumba za ibada akijaribu kujenga taswira ya kuonewa huruma na kuhusisha jina la marehemu John Pombe Magufuli na safari yake ya kisiasa.
“Anajaribu kutuaminisha kwamba Rais Magufuli alimpenda sana. Lakini waliopendwa na Magufuli tunawajua, na baadhi yao wapo humu bungeni. Aache kutumia majina ya viongozi kwa manufaa yake binafsi,” alisema.
Hata hivyo, Simai hakumtaja kwa jina kiongozi anayemhusisha na madai hayo, jambo lililoacha maswali mengi kuhusu mtu anayelengwa na kauli hizo.
Je “Yuda” ni nani?