Naibu gavana nchini Kenya afariki dunia ndani ya ndege

Naibu Gavana wa Kaunti ya Baringo nchini Kenya, Charles Kipng’ok amefariki dunia ndani ya ndege muda mfupi kabla ya ndege kupaa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwenda Mombasa.

Kipng’ok amefariki dunia Jana Jumatano Septemba 14, 2022 jioni ndani ya ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways, ambapo alitarajiwa kuungana na wakuu wengine wa kaunti kwa ajili ya kujitambulisha kwa Baraza la Gavana.

Akizungumza na wanahabari leo Alhamisi Septemba 15, 2022 jijini Nairobi, Gavana wa Kaunti ya Baringo, Benjamin Cheboi amethibitisha kifo cha naibu gavana huyo.

Shirika la ndege la Kenya Airways limethibitisha kuwa abiria aliyepata matatizo ya kupumua alipokuwa akipanda moja ya ndege zake amefariki.

Katika taarifa iliyotolewa jana, KQ ilisema abiria huyo alitangazwa kuwa amefariki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) huku ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Mombasa ikiwa bado ardhini.

“Kenya Airways PLC inasikitika kutangaza abiria wake alipata matatizo ya kupumua jioni hii alipokuwa akipanda KQ612, kuwa amefariki wakati wafanyikazi wa matibabu wa JKIA wakati ndege ikiwa chini,” imesema taarifa ya KQ.

Hili ni tukio la tatu katika kipindi cha wiki nne zilizopita.

Shirika hilo mapema mwezi huu lilithibitisha kwamba abiria aliyekuwa kwenye mojawapo ya safari zake za ndege kuelekea New York nchini Marekani kutoka Nairobi alifariki dunia, ikiwa ni tukio la pili kama hilo kuripotiwa katika muda wa siku tisa.

Mwezi uliopita, iliripoti tukio lingine ambapo abiria alifariki kwenye mojawapo ya ndege zake kutoka New York kuelekea Nairobi.

Chanzo Mwananchi